Na Zillipa Joseph, Katavi
Lishe ni majumuisho ya hatua mbalimbali tokea chakula kinapoliwa na jinsi miili inavyochukua virutubisho na kuvitumia katika kumpatia mlaji afya bora.
Lishe bora kutokana ni ulaji unaofaa, yaani chakula cha kutosha, na cha mchanganyiko chenye virutubisho katika uwiano unaotakiwa. Lishe duni hasababisha utapiamlo ambao huleta madhara ya kiafya.
Serikali imeweka msisitizo katika kuboresha lishe na afya za wananchi wake.
Halmashauri ya Nsimbo iliyopo wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imeweka mkakati wa kuondokana na tatizo la lishe duni kwa kuhakikisha elimu juu ya lishe inaenea katika vijiji vyote kwa kupitia maonesho maalum ya siku ya lishe ya kijiji.
Aidha katika mkakati huo wadau wa halmashauri wamekubaliana kuanzisha bustani za mboga na mashamba ya mazao ya chakula na biashara kwa shule zote za msingi lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi hawakosi chakula wawapo shuleni.
Mzee Hamad Kauzeni ni mkazi wa kijiji cha Songambele, yeye anashauri kila mzazi atoe mchango wa shilingi 1,000/- itakayotumika kuweka ng’ombe wa kulima mashamba ya shule pamoja na kununua mbolea.
Afisa lishe wa halmashauri ya Nsimbo Nickson Yohannes amesema hali ya udumavu katika halmashauri hiyo ni asilimia 32.2 kwa mujibu tafiti ya mwaka 2022 tofauti na mwaka 2015 ambapo ilikuwa asilimia 35.
Ametaja sababu za udumavu kuwa ni pamoja na kutohudhuria kliniki ya mama, baba na mtoto wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua.
Sababu nyingine ni watoto kutopata matone ya vitamin A, elimu ndogo juu ya lishe na familia nyingi kutelekezwa.
Pia Afisa lishe huyo ametoa wito kwa wazazi kuchangia chakula cha watoto shuleni.
“Wazazi wasione kama ni mzigo bali wachukulie kwamba ni sawa na kutoa chakula ambacho mtoto angekula nyumbani mchana” alisema Nickson.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nsimbo Mhandisi Stephano Kaliwa ameshauri wazazi kuhakikisha wanachangia chakula pindi watoto wakifungua shule ambacho kitaendelea kutumika hadi pale shule zitakapofanikiwa kupata mavuno kupitia kilimo cha kujitegemea.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Mhe. Festo Dugange amesema takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano bado ni kikubwa ambapo kwa mkoa wa Kigoma ni 27.1%, Katavi 32.2%, Njombe 50.4%, Songwe 31.9% na Rukwa 49.8%.
Kufuatia hali hiyo shirika la nchini Marekani la USAID limetia mkataba na serikali wa utelekezaji wa mradi wa lishe ili kupunguza udumavu kwa watoto.
Mhe. Dugange amehamasisha ulaji wa chakula mchanganyiko chenye virutubisho na kuzingatia mtindo bora wa maisha.
Aidha amewataka viongozi katika Mikoa na Halmashauri kuzingatia na kudhibiti maradhi yanayochangia matatizo ya lishe na kuimarisha uhakika wa chakula na matunzo bora ya wanawake na watoto.
Katika sera ya Afya ya mwaka 2017 Serikali inahamasisha na kuelimisha jamii umuhimu wa lishe bora. Serikali imedhamiria kuimarisha na kuboresha huduma za lishe nchini.
Tamko la sera hiyo linaeleza kuwa Serikali itaweka mazingira mazuri kwa wadau kushiriki katika kuboresha huduma za lishe na udhibiti wa magonjwa.
Taasisi isiyo ya kiserikali ya LARDEO inayojishughulisha na utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto Kwanza mkoani Katavi imekuwa ikihimiza matumizi ya chakula mchanganyiko kwa watoto hasa wa chini ya umri wa miaka nane.
Filbert Chundu ni Mratibu wa LARDEO anasema mila potofu za kukataa kula mboga za majani hasa kwa wakazi walio kando ya ziwa Tanganyika zinachangia udumavu kwa watoto.
Mkuu wa mkoa wa Katavi Bi. Mwanamvua Mrindoko anasisitiza elimu ya lishe kuendelea kutolewa katika ngazi zote kuanzia mitaa, vijiji hadi kata.
“Hii siku ya lishe ya kijiji ni ya muhimu sana kwa jamii kujifunza makundi ya vyakula na kazi zake” alisema Mrindoko.
Katika hali inayoonyesha kuchangia watoto kupata udumavu mwandishi wa habari hizi ameshuhudia watoto wa chini ya umri wa miezi sita kuanzishiwa chakula wakati wanapaswa kunyonya maziwa ya mama pekee.
Bugoma Anderson ni mkazi wa Mpanda anashauri kuwa elimu ya lishe ingetolewa hata katika maeneo yaliyo mbali na mijini.
Dokta Jonathan Budenu ni mganga mkuu wa mkoa wa Katavi amesema udumavu unasababisha umaskini katika familia.
Amefafanua kuwa mtoto anapopata udumavu akili yake inakuwa nzito katika kufanya maamuzi hali hiyo inamuathiri hata anapokuwa mtu mzima.
Kupitia mwongozo wa programu jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto uliotolewa na Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, jitihada za kushughulikia hali ya lishe nchini zimekuwa na mafanikio makubwa.
Mwongozo huo unafafanua kuwa katika kila watoto kumi hapa nchini walio na umri wa chini ya miaka mitano mtoto mmoja anaripotiwa kuwa na udumavu mkali.
Hii inaashiria kwamba watoto zaidi ya milioni tatu wanaathiriwa na udumavu nchini.
Hivyo basi ni vyema jamii ikaweka msisitizo katika kulisha watoto wao hasa wenye umri wa chini ya miaka nane vyakula vya makundi mchanganyiko ili kuepuka udumavu nchini.