Na. WAF, Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameipongeza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ubunifu wa kutumia kondo la nyuma la akinamama waliojifungua kuzalisha gesi kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine hospitalini.
Dkt. Mollel, ametoa pongezi hizo Tarehe 20 Juni, 2024 wakati akizungumza na watumishi wa sekta ya Afya kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma .
“Nawapongeza sana watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa kutumia kondo la nyuma la mama aliyejifungua na kuliweka kwenye utaratibu maalum kwenye chemba maalum ambalo mwisho wa siku inabadilika kuwa gesi ya kupikia katika mahitaji ya hospitali”, amepongeza Dkt. Mollel.
Amesema watumishi hao wamekuwa wabunifu kwa kuangalia ni maeneo gani yanaiingiza serikali gharama mojawapo ni maeneo ya kuzalisha nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia na mambo mengine muhimu.
Hata hivyo ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kutumia vitu walivyonavyo kuindolea serikali gharama kwa kuhakikisha Huduma bora zinapatikana kwa wanchi wanaowahudumia.
“Leo kondo la nyuma la akinamama wanaojifungua siyo changamoto ya kutuumiza kichwa tutupe wapi leo tunatamani yatoke mengi ili kuweza kuzalisha gesi zaidi kwa matumizi ya hospitali , hongereni sana”, ameeleza Dkt. Mollel
Aidha, Hata hivyo amewapongeza watumishi wa afya nchini na kuwataka kuimarisha ushirikino baina yao ili kuongeza utendaji kazi kwa kuendelea kutoka huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Mollel amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewekeza vya kutosha katika sekta ya afya ambapo mpaka sasa Kituo cha umahiri cha saratani kinatarajiwa kujengwa Dodoma na kusimikwa mtambo mkubwa wa Bilioni 175 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamini Mkapa.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Dkt. Ahmadi Makuwani amesema katika kusherehekea wiki ya Utumishi wa Umma Wizara ya afya inaungana na Wizara nyingine nchini katika kusherekea wiki hii ambapo inakuwa ni kliniki ya masuala ya utumishi wa umma nchini na hufanyika kila mwaka.
Kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika na Serikali watumishi pia wamefanya ubunifu mkubwa kuhakikisha wanaiunga Serikali mkono kwa kazi nzuri iliyofanyika ya uwekezaji katika miundombinu.