Adeladius Makwega-MWANZA
Serikali imesema kuwa Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya(MCSD) kuongeza udahili wa wanachuo wake hadi kufikia maradufu kwa kuwekeza katika Mkoa yote ya kanda ya zima na maeneo jirani.
Kauli hii ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania Dkt. Seleiman Serera alipokuwa akizungumza katika ziara yake ya kikazi na MCSD akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kwimba Juni 19, 2024 mkoani Mwanza.
“Kwa takwimu nilizonazo chuo chetu kina wakurufunzi(wanachuo) wawili tu kutoka wilaya ya Kwimba, kwa hivyo ninawaagiza kuhakikisha kila mnapofanya mazoezi ya vitendo wakati wa likizo wakurufunzi wenu lazima kulenga shabaha muwapange kanda ya ziwa ili muongeze huo udahili na jamii hii kukifahamu chuo.
Mnaweza kuamua kuwa muhula huu wanachuo wote wafanye mazoezi ya vitendo eneo husika, hilo litaongeza ufahamu wa chuo hiki maana kanda ya ziwa inayo vijana wengi wenye sifa za kujiunga na chuo hiki na kipo katika ardhi yao, kanda ya ziwa ni eneo la kimakakati.”
Naibu Katibu Mkuu Serera alisema kuwa kama MCSD kikapata wanachuo hao kutoka kanda ya ziwa, idadi ya wanachuo itakuwa kubwa na siyo 2 kwa 300 bali itaweza kuwa hata 300 kwa 300 au 300 kwa 600.
Akizungumza katika kikao cha ndani na watumishi wa chuo hiki cha umma Katibu Mkuu Serera alisisitiza ushirikiano baina ya taasisi za Serikali Kuu na wilaya ambazo miradi mbalimbali ya serikali inafanyika.
“Hii miradi yote ni wananchi na inapaswa kusimamiwa na viongozi wa wilaya na wananchi wa eneo husika.”
Akizungumza katika Kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Misungwi ambaye ndiye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Bi Johari Samizi alisema
Naibu Katibu Mkuu Serera amewezesha kujenga umoja baina yao, maana Dkt Serera aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya. Mhe Samizi alisema kuwa kwa hakika yeye anafahamu mengi juu ya MCSD.
“Nakubaliana na wewe Naibu Katibu Mkuu kwani miradi yote ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mimi kama Mkuu wa Wilaya ndiye askari wa Mama Samia katika eneo alilonipangiwa, hatuwezi kumuangusha Rais .”
Ziara hii ya Naibu Katibu Mkuu Dkt. Serera ni ya pili kwa chuo hiki ambapo ziara za Dkt Serera zinaonesha kujenga ujirani baina ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, mpaka sasa MCSD kina miradi mikubwa miwili inayogharimu jumala ya shilingi Bilioni 34 za Kitanzania ikiwa miradi ya kimkakati.