Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga ameadhimisha siku ya mtoto wa Afrika kwa kutembelea kituo cha Light In Africa na kuwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapa urithi wa elimu watoto wao ili iweze kuwasaidia kwa miaka ijayo kwani ni jambo lisilo hamishika wala kufilisika.
Sendiga ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambapo ametembelea kituo cha watoto wenye mahitaji maalumu cha Light In Africa kilichopo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.
Amesema urithi wa elimu ni bora zaidi kuliko urithi wa mali kwani mtoto akipatiwa elimu hawezi kufilisika tofauti na mali au rasilimali nyingine inayohamishika na isiyohamishika ila inauzika.
Amesema jamii inapaswa kuishi kupitia kauli mbiu ya siku ya watoto inayosema elimu jumuishi kwa watoto, izingatiwe maarifa, maadili na stadi za kazi.
“Unapompa mtoto urithi wa elimu unakuwa umewekeza jambo kubwa kwenye maisha yake na hata akiwa mkubwa ataitumia elimu hiyo kwa manufaa yake na jamii inayomzunguka,” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa wa Manyara, katika kukitembelea kituo hicho amekabidhi kiasi cha fedha kwa ajili ya kununulia mahitaji muhimu.
“Tumetoa sadaka yetu kwa watoto hawa ili waweze kununuliwa mahitaji muhimu na tunawapongeza wasimamizi na walezi wa watoto hawa kwa namna mnavyokuwa nao,” amesema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, (Marema) Justin Nyari amempongeza mkuu huyo wa mkoa kwa kushiriki siku ya mtoto wa Afrika kwenye kituo hicho.
“Mkuu wetu wa mkoa wa Manyara, amefanya jambo sahihi kujumuika nao kwani hawa watoto wa kituo hiki cha Light in Africa ukiwaona utatoa machozi hivyo wanapaswa kusaidiwa,” amesema Nyari.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Shujaa Baruti amesema amekuwa akijumuika na watu wanaotaka kutoa sadaka kwa watoto hao ambao ni walengwa husika.
“Unapaswa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uzima kwani ukiwaona watoto wa kituo hicho utatoa machozi kwa namna walivyo ila nawapongeza wanaowaea na kuwapa uangalizi wana moyo mkunjufu,” amesema Baruti.