Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya ziara ya kikazi katika mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira kwa lengo la kukagua miradi ya Sekta ya Madini inayosimamiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Ziara hayo imefanyika leo, Juni 15, 2024 katika mgodi huo uliopo katika eneo la Kabulo wilaya ya Ileje mkoani Songwe ambapo Kamati hiyo imekagua miradi mbalimbali katika mgodi huo ikiwemo mradi wa uchimbaji makaa ya mawe, jengo la uzalishaji mkaa mbadala wa kupikia (Coal Briquettes) na maabara kwa ajili ya makaa ya mawe.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. David Mathayo ameitaka STAMICO kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe angalau kufikia uzalishaji wa tani elfu 50 kwa mwezi ili kufikia kiwango kinachoendana na ukubwa wa Shirika.
Aidha, Dkt. Mathayo ameielekeza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo kuisimamia vyema Menejimenti ya Shirika hususan gharama za manunuzi ya mitambo na vifaa mbalimbali ili kutoliongezea Shirika mzigo katika uendeshaji.
Sambamba na hayo, Dkt. Mathayo ameitaka STAMICO kuendelea kutafuta maeneo mapya yenye hifadhi kubwa na ubora wa makaa ya mawe hususan katika mikoa ya Ruvuma na Njombe ili kuongeza tija katika uzalishaji wa madini hayo na kuhakikisha wanalipa madeni wanayodaiwa na wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steve Kiruswa amesema Wizara ya Madini imepokea ushauri wa kamati na itasimamia vyema utekelezaji wake ili kuongeza tija na manufaa katika uzalishaji wa madini nchini.
Aidha, Dkt. Kiruswa amesema kuwa Vision 2030 itaongeza wigo kwa watanzania kushiriki katika mnyororo mzima katika Sekta ya Madini unaounganisha sekta hiyo pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara likiwemo STAMICO na Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa lengo la kuongeza kwenye sekta hiyo.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO Meja Jenerali (Mst) Michael Isamuhyo ameishukuru Kamati ya Bunge kwa kufanya ukaguzi katika eneo la mradi wa uchimbaji makaa ya mawe wa Kabulo-Kiwira.
Pia, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Deusdedith Magala amesema STAMICO inaendelea kuthamini mchango wa Wafanyakazi wake wote katika kuleta ubunifu na uthubutu jambo lililopelekea Shirika kufanikiwa sambamba na kuanza uzalishaji wa bidhaa mpya ya Mkaa mbadala wa kupikia ujulikanao kwa jina la Rafiki Briquette.
Katika hatua nyingine, Magala amesema, kutokana na ukarabati na uwekezaji ulifanywa na STAMICO, mauzo yameongezeka kutoka shilingi 221,389,014 mwaka 2017/18 mpaka 6,144,184, 964.64 katika Mwaka wa Fedha 2022/23 huku Shirika likilipa kodi mbalimbali pamoja na tozo kwa kiasi cha shilingi 950,260,995.87.