Mwezeshaji wa programu ya Tehama, Suna Salumu, akiwaelekeza wanafunzi wa kike katika Chuo Cha Ualimu Butimba, Mwanza, wanaoshiriki katika programu maalum ijulikanayo kama ‘Code Like A Girl’ yenye lengo la kuwahamasisha wanafunzi wa kike kupenda masomo ya Sayasi, Hisabati, na Teknolojia (STEM). Mpango huu unaofadhiliwa na Vodacom Tanzania Foundation, unalenga kuwafikia zaidi ya wanafunzi wa kike 2,000 katika mafunzo yaliyofanyika katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Arusha, Dodoma, na Dar es Salaam.
……..
Katika kusapoti juhudi za wasichana kuingia kwenye masomo ya Sayansi na kutumia teknolojia zaidi ya wasichana 2000 wenye umri kati ya miaka 14-18 kutoka shule za sekondari zilizopo mikoa ya Mwanza,Mbeya Arusha,Dodoma na Dar-es-saalam wanatarajia kunufaika na mradi wa ‘Code Like a girl’ wenye lengo la kuhamasisha masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknolojia(STEM).
Akizungumza wakati wa ufundishaji wa masomo hayo Juni 14,2024 katika chuo cha Ualimu Butima,Mratibu wa mradi huo kutoka Tanzania Data Lab(DLab),Somoe Mkwachu amesema mradi huo wanashirikiana na kampuni ya Vodacom.
Amesema wameamua kuja na mradi huo ili kuhamasisha watoto wengi wa kike kupenda masomo ya Hisabati, Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuweza kutimiza ndoto zao katika elimu.
‘’Katika mradi wetu tunafundisha wanafunzi kutumia Kompyuta katika masomo yao pia. Huwa tunachagua wanafunzi kuanzia 70 kutoka shule pendekezwa na kuwapa elimu ya kompyuta kwa muda wa siku tano haswa wakati wanapokuwa Likizo’’ amesema.
Amesema katika mafunzo waliotoa katika mkoa wa Mwanza kwa awamu mbili wamefanikiwa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi 192 kutoka shule za sekondari Nyakurunduma, Butimba day,Mkolani,Shamaliwa,Nasco na Musabe.
Amesema programu hiyo huwa inafanyika katika kipindi cha likizo za shule kama vile mwezi wa sita, likizo fupi ya mwezi wa 9 pamoja na mwezi wa 12.
Amepongeza juhudi za wanafunzi hao wanapokuwa wanafundishwa masomo hayo wamekuwa wakionyesha bidii kubwa sana ya kutaka kujua masomo.
Naye Meneja mwandamizi wa Vodacom, Kanda ya Ziwa Victoria Chale amesema lengo la kampuni yao kuhamasisha watoto wa kike kutumia teknolojia ili waweze kujua hata wao wanaweza masomo ya Sayansi.