Vyama vya siasa vimeunga mkono rasimu ya kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, ambapo leo wawakilishi kutoka vyama 19 wamekutana jijini Dodoma kupitia na kutoa maoni yao kuhusu rasimu za kanuni nne za kusimamia uchaguzi huo.
Rasimu hizo ni za kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka ya mji mdogo, kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa, kanuni za uchaguzi wa serikali za mtaa katika mamlaka ya wilaya na kanuni za uchaguzi wa serikali za mtaa katika mamlaka za miji, zote za mwaka 2024.
Akifungua kikao hicho, Naibu Waziri wa TAMISEMI (Elimu), Mhe. Zainab Katimba amesema kuwa rasimu ya kanuni hizo imezingatia maoni na michango iliyotolewa na wadau mbalimbali, huku akisisitiza kuwa pia ni utekelezaji wa azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki kwa kuzingati misingi ya falsafa ya 4R.
Wachangiaji kutoka vyama vingi wamempongeza Rais Samia kwa hatua ambazo amaeendelea kuchukua ikiwemo marekebisho ya sheria za uchaguzi, kanuni na miongozo, kwani ni mambo ambayo wamekuwa wakiyapigia kelele kwa miaka mingi na hayakuwa yamefanyiwa kazi.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa vyama wametoa mapendekezo mbalimbali ili kuboresha kanuni hizo, ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda kimependekeza ili kuhakikisha kuwa wasimamizi wa uchaguzi wana sifa zinazostahili na zinazoeleweka vyema wanapendekeza kigezo zaidi cha historia ya uadilifu, uzoefu katika masuala ya uchaguzi ambavyo vitasaidia kuhakikisha msimamizi wa uchaguzi ni mtu mwadilifu na mwenye uzoefu wa kusimamia uchaguzi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika amependekeza masuala mbalimbali ikiwemo muda wa kampeni kuongezwa hadi angalua siku 14, tofauti na siku saba za sasa, uandikishaji wa wapigakura ufanyike mara moja ili kubana fedha za umma na pia kusiwe na ulazima wowote wa kutaka msimamizi wa uchaguzi kuwa mtumishi wa umma bali watu watume maombi, na vyama viwe na fursa ya kuweka pingamizi.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Shaweji Mketo amependekeza maboresho yafanyike kuondoa ulazima wa mawakala wa uchaguzi kuapishwa na hakimu badala yake waapishwe na wasimamizi wa uchaguzi.