Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke(TRRH) imeanza rasmi kutoa huduma za usafishaji damu (dialysis) leo tarehe 14 Juni 2024, ikiwa ni mara ya kwanza kwa hospitali hiyo kutoa huduma hii maalumu itakayo hudumia wananchi wenye changamoto ya figo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mfawidhi wa Hospitali, Dkt. Joseph Kimaro, amethibitisha kuanza rasmi kwa huduma hiyo na kusema kuwa hii ni siku muhimu kwa hospitali, kwani huduma hiyo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu.
Amesema kuwa hospitali imepata mashine kumi za usafishaji damu zilizonunuliwa kwa kutumia mapato ya ndani. Dkt. Kimaro ameeleza kuwa huduma hii itasaidia wagonjwa wenye matatizo ya figo wanaoishi maeneo jirani kama vile Kigamboni, Kuranga, na Pwani, ambapo hakuna hospitali inayotoa huduma kama hiyo.
Aidha, Dkt. Kimaro amesema kuwa utekelezaji wa huduma hii sio tu hitaji la Hospitali ya Temeke bali ni mpango wa serikali ya Tanzania, ambayo inalenga kufikisha huduma za kibingwa na bingwa bobezi kwa wananchi. Huduma hii mpya itapunguza foleni na changamoto za umbali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Dkt. Kimaro ametoa shukrani kwa Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam(TPA) kwa kuwezesha ukarabati wa jengo hilo na kununua televisheni zitakazosaidia wakati wa kutoa huduma. Pia amewataka wananchi kuendelea kufanya mazoezi na kufuata ushauri wa madaktari ili kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kwani dawa zisipotumika kwa usahihi zinaweza kusababisha changamoto za figo.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Dkt. Farida Ntonga, ameshukuru uwepo wa mashine hizo na kusema kuwa timu ya madaktari na wauguzi wamepokea mafunzo ya kutosha, hivyo wananchi wawe na imani na wataalamu hao.
Amesema mwaka jana hospitali ilipokea wagonjwa takribani 200 ambao walihitaji rufaa kwenda Muhimbili, lakini sasa kutokana na huduma hii mpya, rufaa hizo zitapungua na wagonjwa watapata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke(TRRH).
Bw. Humphrey Tarimo, baba mkubwa wa mgonjwa wa kwanza kuhudumiwa, ameelezea furaha yake kwa huduma hiyo kusogezwa karibu na makazi yao.
Amesema walikuwa wakipata changamoto za usafiri kutokana na umbali wa hospitali hivyo anaupongeza uongozi wa hospitali kwa ukarimu na utashi wao wa kujali wagonjwa. Pia ametoa shukrani kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusogeza huduma hizi karibu na jamii na ameomba huduma hizi ziendelee kusambaa maeneo mengine ili kusaidia wananchi zaidi.