Na. Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini leo wamefanya kikao cha ujirani mwema huko katika mpaka wa Namanga, Wilaya ya Longido mkoani Arusha kwa ajili ya kuimarisha mahusiano mazuri pamoja na namna bora ya kudhibiti uhalifu katika maeneo ya mipakani.
Akiongoza kikao hicho, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Simon Pasua amebainisha kuwa Jeshi hilo linafanya vikao hivyo kujadiliana kwa pamoja na kuwekeana mikakati ya kudhibiti vitendo vya kihalifu hususani ya utoroshwaji wa mifugo kwenda nje ya Nchi bila kibali.
Aidha amesema kikao hicho cha ujirani mwema kimekua na manufaa mengi ikiwa ni pamoja kuimarishwa kwa mahusiano baina ya nchi hizo ambapo kwa sasa mwamko ni mkubwa katika utoaji wa taarifa za kihalifu.
Katika hatua nyingine Kamanda Pasua ametoa wito kwa Wafugaji kote Nchini kuhakikisha wanatumia vyema maeneo ya malisho hususani katika msimu huu ambao unaelekea kiangazi ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara ambayo inaweza kujitokeza huko baadaye.
Kwa upande Wake Afisa Mfawidhi wa Mifugo toka Nchini Kenya Dkt. James Wahungu amebainisha kuwa vikao hivyo ni muhimu sana na vitakua vinafanyika kila mwezi ambapo mbali na kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili, vitasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji na wafanyabishara wa mifugo.
Naye Bwana Timoteo Laizer ambaye ni mfugaji na mfanyabiashara wa mifugo amebainisha kuwa kikao hicho ni kizuri kwani kimesaidia kuwapa elimu mbalimbali katika suala zima la kufuata taratibu za upelekaji wa mifugo nje ya nchi na kuahidi kwenda kutoa hamasa kwa wafanyabiashara wenzake kuepuka kupitisha mifugo kwa njia za magendo.
Kwa upande wake Bwana John Vicent ambaye ni Wakala wa kusafirisha mifugo maeneo ya mpaka wa Namanga amesema changamoto kubwa inayowafanya wafugaji na wafanyabishara kutorosha mifugo yao bila kuwa na vibali ni ukosefu wa elimu na uelewa juu ya njia sahihi za kupata vibali.