Serikali ipo katika majadiliano na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hatua hiyo inafanyika kuwezesha Tanzania kunufaika na mkopo nafuu kupitia dirisha la Resilience and Sustainability Facility (RSF). Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameliarifu Bunge jijini Dodoma leo Juni 13, 2024 wakati akiwasilisha Bajeti ya Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Amesema kwa kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza programu za uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa kufanya mazungumzo na Washirika wa 56 wa Maendeleo ili kupata fedha za kukabiliana na changamoto hiyo.
Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Waziri Nchemba amezielekeza taasisi zote kujumuisha masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira wakati wa kupanga na kutekeleza sera na programu mbalimbali
Aidha, amesema katika kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, amempongeza Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kupunguza uchafuzi wa mazingira kupitia hewa ya kaboni.
Mheshimiwa Rais katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Dubai mwaka 2023 (COP 28) alizindua rasmi mpango wa utekelezaji wa Mradi wa Nishati Safi ya kupikia kwa Wanawake Afrika – AWCCSP) ambao una lengo la kuleta mageuzi ya nishati ya kupikia na kumkomboa mwanamke na kulinda mazingira yetu,” amesema.
Ameongeza kuwa Dkt. Samia alizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034) ikiwa ni moja ya hatua za awali za kitaifa za utekelezaji wa programu hiyo wenye kulenga kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watanzania kwa kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu 57 ya uhakika ya nishati safi ya kupikia.
Hivyo, Dkt. Nchemba ametoa rai kwa wananchi na wadau wote kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika jitihada za kufanikisha utekelezaji wa mkakati huu.