Na. Abel Paul, Jeshi la Polisi- Arusha.
Kuelekea siku ya mtoto wa Afrika Jeshi Polisi Mkoani Arusha limeendelea kuyakumbuka makundi mbalimbali katika jamii kwa kutoa elimu na michango ambapo leo Polisi Wilaya ya Kipolisi Murieti wametoa elimu hiyo katika kituo cha Watoto wenye usonji Mount of Joy Foundation kilichopo eneo la murieti jijini Arusha.
Akiongea mara baada ya kutoa elimu hiyo Mkuu wa kituo cha Polisi Wilaya ya kipolisi Murieti Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Taus Mbalamwezi amesema kuwa kuelekea siku hiyo ya mtoto wa afrika wameona ni vyema kufika katika kituo hicho na kutoa elimu Pamoja na zawadi ambazo zitawapa furaha Watoto wa kituo hicho.
ASP Taus ameongeza kuwa Jamii inapaswa kutambua kuwa ukatili ni Pamoja na kumnyima haki mtoto ya kusoma na kupata elimu huku akiwataka wazazi wenye tabia ya kuficha Watoto wenye usonji waache kuwaficha Watoto na badala yake wawafikishe katika vituo husika ili wapate msaada.
Kwa upande wake Christine Godderz ambaye ni mwalimu kutoka nchini ujerumani amesema yupo katika kituo hicho kwa ajili ya kujitolea kufundisha Watoto hao wenye changamoto ya usonji huku akibainisha kuwa anatumia nafasi hiyo pia kujifunza na kubadilishana uzoefu na maarifa.
Nae Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kipolisi Murieti Mkaguzi msaidizi wa Polisi A/INSP Ngolo Matogolo amesema kuwa wamefika katika kituo hicho ikiwa ni mwendelezo wa kutoa elimu kwa jamii yote juu ya vitendo vya ukatili.
Mwenyekiti wa mtaa wa Ffu Murieti jijini Arusha Veronika Simon licha ya kulishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha amesema vitendo vya ukaili vinapaswa kupingwa kwa nguvu zote huku akitoa wito kwa jamii kutokuyasahau makundi hayo ya uhitaji katika jamii.