Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Mh. Jacobs Mwambegele akifungua mafunzo ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kuhusu uboreshaji wa Daftari la Wapiga kura , Sheria na Kanuni zake ambapo uzinduzi unatarajiwa kufanyika Julai Mosi mwaka huu mkoani Kigoma.
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari kalutoka vyombo mbalimbali katika mafunzo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Milimani City jijini Dar es salaam.
…………………
Na Sophia Kingimali.
Uzinduzi wa uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura nchini linatarajiwa kuzinduliwa rasmi Julai 1,2024 mkoani kigomo huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa huku kauli mbiu ikiwa ‘kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora’.
Akizungumza leo Juni 13,2024 jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa Tume huru ya taifa ya Uchaguzi (INEC) na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele amesema maandalizi kuelekea uboreshaji huo yamekamilika huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kushiriki katika kuboresha taarifa zao.
“Siku ya uzinduzi huo ndio siku rasmi ya kuanza kwa zoezi hilo kuanza kwa mkoa wa Kigoma kisha mikoa mingine ya Katavi na Tabora na kufuatiwa na Kagera na Geita”,Amesema Jaji Mwambegele.
Amesema uboreshaji wa awamu ya kwanza utafanyika kwenye mizunguko 13 ambapo zoezi litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo huku zoezi likitarajiwa kukamilika Machi,2025.
Amesema uboreshaji huu utatumia teknolojia ya BVR Kits katika uchukuaji wa alama za vidole,picha na saini.
Sambamba na hayo ametoa rai kwa Wazee,wagonjwa,walemavu na wamama wajawazito na wenye watoto wadogo kujitokeza kwa wingi kuboresga taarifa zao kwani mazingira ni mazuri na wametoa kipaumbela kwa watu hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima akizungumzia idadi ya wapiga kura wanaotarajiwa kupiga kura amesema wapiga kura wapya wanaotarajiwa ni 5,586,433 kati ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/20.
Amesema wapiga kura 4,369,531 wanatarajia kuboresha taarifa zao wakati wapiga kura 594,494 wanatarajiwa kuondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendeleo kuwepo kwenye daftari hilo ambapo baada ya uboreshaji inatarajiwa kuwa Daftari litakuwa na jumla ya wapiga kura 34,746,638.
“Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikua na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari mwaka 2019/20 lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha kuwa wapiga kura”,Amesema Kailima.
Sambamba na hayo amesema Tume tayari imekamilisha maandalizi yote ikiwemo vituo vya kuandikishia wapiga kura ambapo vipo vituo 40,126 nchi zima Tanzania bara na Zanzibar.