Mkurugenzi Mtendaji wa Upendo Media Neng’ida Johanes (kushosho) akiwa na Naibu Katibu Mkuu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Mchungaji Wilbroad Mastai wakati wakizungumza na waandishi wa habari leo Juni 13, 2024 jijini Dar es Salaam kuhusu kuhusu Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu linalotarajiwa kufanyika Juni 15, 2024 katika Viwanja vya Tanganyika Packers vilivyopo Kawe, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Mchungaji Wilbroad Mastai akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 13, 2024 jijini Dar es Salaam kuhusu kuhusu Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu linalotarajiwa kufanyika Juni 15, 2024 katika Viwanja vya Tanganyika Packers vilivyopo Kawe, Dar es Salaam.
…..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wazazi na walenzi kutoka dini na madhehebu mbalimbali wametakiwa kuwapa ushirikiano vijana ili waweze kushiriki Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu linalotarajiwa kufanyika Juni 15, 2024 katika Viwanja vya Tanganyika Packers vilivyopo Kawe, Dar es Salaam.
Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu mwaka huu linafanyika katika Viwanja vya Tanganyika Packers kwa sababu Uwanja wa Uhuru uliozoeleka unafanyiwa ukarabati, hivyo usingeweze kutumika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 13, 2024 jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Mchungaji Wilbroad Mastai, amesema kuwa waimbaji watakaoshiriki katika tamasha la twen’zetu kwa Yesu ni Rose Mhando, Neema Gospel Choir, Agape Gospel Band, Franc Jamarack, Boaz Danken, Kibonge wa Yesu.
Waimbaji wengine ni Hype Squad, Kariakoo KKKT Praise Team pamoja na kwaya nyengine sita zinazounda majimbo ya KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
“Lengo la Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu ni kuwabadilisha vijana kuwa na mtazamo chanya katika kumjua Mungu katika uchumi na uzalendo kwa Taifa lao” amesema Mchungaji Mastai.
Mchungaji Mastai amefafanua kuwa tamasha hilo kwa mwaka huu pia litafanyika katika Mkoa wa Mbeya Juni 28, 2024 katika Uwanja wa Sokoine pamoja na Mkoa Shinyanga katika uwanja wa Kambarage Agosti 10, 2024.
Amesema kwa kipindi cha miaka 11 wameona vijana wengi wakibadilisha maisha kupitia tamasha hilo ambalo limekuwa msaada katika kufata njia rafiki zinazompendeza Yesu.
Mchungaji Mastai amesema kuwa Tiketi kwa ajili ya kushiriki zinapatikana kwa shilingi 5,000 pamoja na T- Shirt kwa gharama ya shilingi 20,000.
“Nawashukuru viongozi wa kanisa, wadhamini pamoja na wadau mbalimbali kwa kushirikiana kuwezesha kufanikisha tamasha la twen’zetu kwa Yesu mwaka 2024” amesema Mchungaji Mastai.
Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu mwaka huu limebeba kauli mbiu isemayo ‘Be the light’ ambapo linatoa nafasi kwa washiriki kuimba na kucheza pamoja na kupata mafundisho kutoka kwa Mnenaji Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati (Singida) Dkt. Syprian Yohana Hilint.
Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu lilianza kufanyika mwaka 2014 mpaka sasa limepiga hatua kubwa kwa kukusanya maelfu ya vijana wa dini na madhehebu mbalimbali wakishiriki kila mwaka kutoka mikoa mbalimbali.