Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Godfrey Mnzava,akikabidhi mafuta ya kupaka kwa mwanafunzi wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko wilayani Tunduru Bihail Hakimu wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea Hospitali ya wilaya Tunduru kwa ajili ya ufunguzi,kulia Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Sabina Lipukila.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Godfrey Mnzava kulia akikabidhi Televisheni kwa wanafunzi wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko wilayani Tunduru iliyotolewa na Halmashauri ya wilaya kupitia mradi wa ugawaji vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa ajili ya kuwawezesha katika masomo yao.Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko wilayani Tunduru,wakimsikiliza Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Mnzava wa pili kushoto,baada ya kiongozi huyo kukagua mradi wa ugawaji vifaa kwa wanafunzi na watu wenye mahitaji maalum jana.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
WITO umetolewa kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu,kutowaficha watoto wao ndani badala yake wahakikishe wanawapeleka shule ili waweze kupata haki yao ya msingi.
Hayo yamesemwa jana na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava alipokuwa akizungumza na wanafunzi,wazazi, wananchi na viongozi wa wilaya ya Tunduru baada ya kushiriki zoezi la kugawa vifaa kwa makundi yenye mahitaji maalum wilayani Tunduru.
Mnzava amesema,zipo shule maalum kwa ajili ya watoto hao kwa hiyo kufanya hivyo ni sawa na unyanyasaji na kumnyima mtoto haki yake ya msingi ya kupata elimu.
Amewaomba wadau wa maendeleo wa ndani nan je ya nchi,kushirikiana na serikali katika kuwapatia huduma stahiki wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika suala la kujifunza kwa ngazi zote za elimu.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko Sabina Lipukila alisema,Halmashauri ya wilaya Tunduru baada ya kuona uhitaji mkubwa wa watu wenye ulemavu, imekuwa ikitenga fedha kutoka kwenye mapato yake ya ndani kwa kila mwaka ili kuweza kuwahudumia kwa kuwapa mahitaji yao ya msingi.
Aidha alisema,shirika la kalamu Education Foundation limetoa vifaa mbalimbali vyenye gharama ya Sh.milioni 2,725,000 ili kusaidia watu wenye mahitaji maalum ambavyo ni viti vya magurudumu mawili 5,kofia 15 na fulana 50.
Mwanafunzi wa shule hiyo Bihail Hakimu,ameishukuru serikali kwa kuwajali na kuomba wadau wengine kujitokeza kuwasaidia ili waweze kutimiza ndoto zao.