Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Dodoma.
Mahitaji ya msingi ya binadamu ni chakula, malazi na mavazi. Binadamu akiyapata mahitaji haya, anakuwa amekidhi mahitaji muhimu na hivyo kuendelea na mchakato wa kutafuta mahitaji mengine ya ziada kwa ustawi wa maisha yake.
Hitaji la chakula kwa mfano linakamilika pale ambapo chakula kinakuwa kimeandaliwa na kupikwa vyema tayari kwa kuliwa. Ili chakula kiive ni lazima kipikwe kwenye nishati ya kupikia kama vile kuni, mkaa, jiko la gesi au umeme na aina nyingine ya nishati kama mafuta ya taa, jua na kadhalika.
Hivyo, kukamilika kwa chakula kunategemea matumizi ya nishati ya kupikia katika maandalizi yake. Kutokana na hatua za kimaendeleo hasa nyanja za sayansi na teknolojia, utunzaji wa mazingira na kulinda afya za binadamu, upo umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia kama vile majiko yanayotumia gesi na umeme na kuachana kabisa na nishati chafu kama ya kuni na mkaa.
Kwa miaka mingi hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania, nishati chafu ya kuni na mkaa imekuwa ndiyo inatumika kwa asilimia kubwa kupikia mijini na vijijini. Matumizi makubwa ya kuni na mkaa yamekuwa na athari hasi katika jamii kutokana na kuharibu mazingira, kuhatarisha afya za binadamu na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.
Katika mambo ambayo naona Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ataacha alama isiyofutika Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla na kufanya jina lake kuandikwa kwa wino wa dhahabu wakati huu akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu ni pamoja na hili la harakati anazozifanya kupambania kufanikisha mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Tanzania na Bara la Afrika.
Zipo harakati nyingi ambazo Rais Samia anafanya ambazo bila shaka zitaacha alama kubwa kama vile kuwarejesha shule wanafunzi waliopata changamoto mbalimbali shuleni ikiwemo mimba, kuhamasisha vijana wakiwemo wasomi kushiriki kwenye kilimo cha kisasa kupitia Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), maboresho ya mitaala ya elimu inayojielekeza kwenye kuwawezesha watoto kumaliza shule wakiwa tayari wana ujuzi fulani na mengine lukuki.
Lakini leo imenipendeza kuangazia hili la nishati safi ya kupikia. Harakati anazozifanya Rais Samia katika eneo hili pekee zinaacha alama kubwa katika uongozi wake na hii ndiyo sifa ya kiongozi bora – kuacha alama.
Jambo hili la kiongozi kuacha alama amelisema pia Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa jijini Dar es Salaam katika mahafali ya saba wakati akiwatunuku astashahada na vyeti wahitimu 198 katika Taasisi ya Uongozi ambapo amewashauri waliohitimu uongozi kuwa na mipango na mawazo yatakayowezesha kuacha alama katika uongozi wao pale watakapomaliza muda au kuhamishwa.
“Watu watakukumbuka kwa lipi katika uongozi wako. Tujitahidi kuacha alama. Viongozi lazima wawe tayari kila wakati kutafuta suluhu za changamoto zinazoendelea kama vile umaskini, mabadiliko ya tabianchi, ujinga, shida ya chakula, magonjwa na mambo mengine wajikite kutatua kero zinazojitokeza,” alisema Kikwete.
Ni ukweli kuwa Rais Samia ameona changamoto zinazosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa, ndiyo maana akachukua hatua za kuwa kinara wa kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia.
Kwa mfano, kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Dk. Selemani Jafo, zaidi ya watu 32,000 hufariki dunia kila mwaka nchini kutokana na matumizi ya nishati chafu huku kila mwaka nchi ikipoteza zaidi ya hekta 469,420 za misitu kutokana na uharibifu unaochangiwa na ukataji miti kwa ajili ya kupata nishati chafu ya kupikia.
Ikumbukwe kuwa matarajio ya serikali ni kuwa hadi kufikia mwaka 2034, zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia. Miaka 10 ijayo kuanzia sasa si mbali, ndiyo maana Rais Samia amekuwa akipaza sauti ndani na nje ya Tanzania kupigania matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akiwa kwenye Mkutano Mkuu wa Nishati Safi ya Kupikia uliowakutanisha Marais, Viongozi na Wadau mbalimbali wa Afrika katika Makao Makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) jijini Paris, Ufaransa, Rais Dk. Samia alisema zaidi ya Waafrika milioni 900 wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia, jambo linalochangia uharibifu wa mazingira, upotevu wa bioanuai na athari za kiafya.
Katika Mkutano huo, Rais Samia alisisitiza kuwa kuongezeka kwa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia itasaidia wanawake kupata fursa zaidi kushiriki shughuli nyingine za kiuchumi, kupunguza umaskini na usawa wa kijinsia.
UTASHI WA KISIASA
Hakuna shaka kuwa Rais Samia amedhamiria kuiona Tanzania na Afrika ikiachana na nishati chafu na kutumia nishati safi na ndio maana kila anapopata jukwaa la kuongea na wananchi, ndani na nje ya nchi amekuwa akisisitiza ajenda ya nishati safi ya kupikia.
Kwa mfano, Mei 8, 2024, Tanzania ilizindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ambapo mkakati huo umekusudia kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ifikapo mwaka 2034 yaani miaka 10 ijayo kuanzia sasa.
Katika Mkutano huo nchini Ufaransa, Rais Samia alisema; “Serikali imelipa umuhimu suala la nishati safi ya kupikia ambapo katika kuyafikia malengo hayo bajeti kuu ya serikali imeweka kipaumbele katika kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo sambamba na kuwainua wanawake.”
Wiki iliyopita, akiwa katika ziara ya siku sita nchini Korea Kusini Samia pia aliingiza ajenda ya nishati safi ya kupikia akiitaka nchi hiyo ambayo imepiga hatua kimaendeleo kuona namna itakavyoweza kusaidia katika suala zima la nishati safi ya kupikia.“Kwa kuwa nimekuwa Rais Mtendaji pekee katika ukumbi huu sasa hivi, lazima nizungumze kuhusu ajenda muhimu ya Afrika na suala la mwanamke wa Afrika… Hili ni suala la kuwekeza katika nishati safi na salama ya kupikia,” alisema.
Alisema Tanzania inapenda kusisitiza hitaji la kuimarisha ubia katika ushirikiano huu ili kuendeleza nishati safi ya kupikia. Alisema uwekezaji katika nishati safi ya kupikia siyo tu utapunguza utoaji wa hewa chafu na kulinda misitu bali pia unapunguza vifo vinavyotokana na matatizo ya upumuaji na kuwawezesha wanawake ambao ndio wapishi kufanya kazi zao kwa usalama zaidi. “Ajenda ya uwekezaji katika nishati safi ya kupikia Afrika pia unatoa fursa za kukua kiuchumi katika maana ya kutafuta ufumbuzi wa upatikanaji wa niashati safi ya kupikia Afrika,” alisema.
Alisema Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dk. Akinwumi Adesina na yeye, wemekuwa wakiifanyia kazi ajenda hiyo ili kupata fedha na kwa msingi huo akaiomba Serikali ya Jamhuri ya Korea kujiunga nao katika suala hilo muhimu.
Dhamira ya Rais Samia ya kutaka ajenda ya nishati safi ya kupikia ifanikiwe Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla imewafanya wabunge, watu binafsi, kampuni binafsi na taasisi zisizo za serikali (NGOs) kutoa misaada wa majiko ya gesi bure kwa mama lishe na wajasiriamali wengine kama mkakati wa kuepukana na matumizi ya nishati chafu. Jambo hili limefanyika na linaendelea kufanyika nchi nzima katika kumuunga mkono Rais Samia na ajenda ya nishati safi ya kupikia.
BWAWA LA NYERERE NA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Serikali inatarajia kutumia Shilingi trilioni 6.6 hadi kukamilisha mradi wa Bwana la Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) ambapo mradi huo unatarajiwa kuzalisha megawati 2115 za umeme ambazo zitasaidia sana kupunguza tatizo la umeme nchini na kuchangia maendeleo ya viwanda na uchumi kwa ujumla.
Nishati safi ya kupikia inahusisha pia matumizi ya majiko ya umeme, kwahiyo kukamilika kwa mradi huu wa umeme kutasaidia pia kuongeza wigo wa matumizi ya nishati safi ya umeme.
Ushauri wangu kwa serikali ni huu, Mradi wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere utakapokamilika na kuzalisha megawati zote 2115, serikali ipunguze bei ya umeme ili kuwawezesha Watanzania wengi kutumia nishati safi ya majiko ya umeme katika kupikia huku wakichanganya na majiko ya gesi ili kutokomeza kabisa matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa.
Kusema ukweli, asilimia kubwa ya Watanzania, hasa waishio mijini wana umeme lakini kwa nini hawatumii majiko ya umeme? Bila shaka sababu kubwa ni gharama kubwa ya umeme. Hata kwenye nyumba zetu nyingi hizi za kupanga si rahisi kukuta matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia yakiruhusiwa. Hata mwenye nyumba akikubali si rahisi wapangaji wenzako wakakubali!
Bei ya umeme na gesi vinapaswa kuwa chini kuliko kuni na mkaa ili wananchi waone umuhimu wa kutumia nishati safi ya bei nafuu na kuachana kabisa na nishati chafu katika kupikia. Kufanyike pia utaratibu wa gesi ambao utawezesha mtu kununua gesi hata akiwa na Sh 1000, kwa maana hiyo wahusika waangalie uwezekano wa hilo.
Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kusambaza umeme mijini na vijijini, hali inayoifanya Tanzania kuwa kinara Afrika kwa usambazaji wa umeme kwa wananchi. Na ndiyo maana Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia (WB) nchini, Nathan Belete amesema Benki hiyo inatambua kazi nzuri zinazofanywana Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika masuala ya nishati.
“Hapa Afrika, Tanzania ni mfano mzuri katika usambazaji wa nishati ya umeme kwa wananchi. Tumejipanga kuwa na mazungumzo zaidi na kuona namna bora zaidi ya kusaidia katika masuala ya nishati safi ya kupikia kwa kufadhili na kuhusisha sekta binafsi kwa kuangalia fursa zilizopo,” amesema Belete.
Ni jambo la faraja kuona juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kusambaza nishati ya umeme kwa wananchi zinatambulika kitaifa na kimataifa. Kwahiyo, umeme huo unaosambazwa kwa wananchi haupaswi kuwa ni kwa ajili ya kupata mwanga usiku, kuangalia runinga na kusomea tu, bali pia uwe ni chanzo cha nishati safi ya kupikia.
Na hii, kama nilivyokwisha sema, itafanikiwa endapo bei ya umeme itashuka kwa kiasi kikubwa hasa baada ya kukamilika mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere litakalozalisha megawati 2115 na pia kuibuliwa na kuendelezwa kwa vyanzo vingine vipya vya nishati ya umeme ukiwemo umeme wa jotoardhi unaotafitiwa kule Mbeya.
Rais wangu, Dk. Samia, nikutie moyo uendeleze mapambano haya ili kufikia mafanikio makubwa kabisa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Ninawaomba Watanzania wenzangu wakiwemo wapinzani wako kisiasa wakuunge mkono angalau hata katika hili. Haiwezekani wao wawe wanakalia kulalamika tu na kutafuta tu makosa wakati mwingine kwa tochi bila kuunga mkono mambo mazuri kama haya na huo ndio uungwana.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.