………………
Na Sixmund Begashe – Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii, imezidi kuongeza kasi katika uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za misitu nchini, ili zitumike kwa faida ya kizazi kilichopo na kinacho kuja.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma kwenye ufunguzi wa warsha ya wadau wa sekta ya Misitu na elimu (NACTVET) iliyolenga kupitia mitaala kwa Taasisi ya Mafunzo ya Misitu, Olmotonyi, chuo ambacho kinaendeshwa chini ya Wizara ya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Misitu nchini, Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Misitu Bw. Selebon Mushi, amesema kuwa uamuzi wa kuendesha warsha hii unaonyesha nia na dhamira ya wizara hiyo, katika kuhakikisha kuwa rasilimali zote za misitu nchini zinalindwa na kusimamiwa vyema.
Bw. Mushi ameongeza kuwa warsha hiyo inalenga kukusanya mawazo na uzoefu kutoka kwa wadau hao utakaosaidia katika kuandaa mtaala ambao utawapa wasimamizi wa ngazi ya kati ujuzi wa kuanzisha, kuendeleza, kusimamia na kutekeleza sheria, kanuni na miongozo mbalimbali kuhusu sekta ya misitu.
Aidha Bw. Mushi ameongeza kuwa Dunia inakabiliwa na changamoto kubwa katika uhifadhi wa misitu kutokana na ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi unaohitaji rasilimali za misitu na ardhi hivyo, changamoto hizi husababisha uvamizi wa ardhi ya misitu.
Akielezea kuhusu mkakati wa Wizara kupitia Chuo cha Misitu, Olmotonyi (FTI), Afisa Utalii Mkuu Kitengo cha Utafiti na Mafunzo Bw. Josephat Msimbano, amesema, Wakufunzi wamefanya kazi kubwa ya kukusanya taarifa kutoka kwa wadau kwa ajili ya mapitio ya mitaala ili kuboresha ushiriki wa wanafunzi na hatimaye kuimarisha ubora mazingira wezeshi kwa wanafunzi kujifunza.
“Hii ina maana kwamba wanafunzi wataondoka chuoni wakiwa na ujuzi na maarifa ya teknolojia ya kisasa ili kufanya kazi kwa ufanisi katika kuhifadhi na kusimamia misitu yetu”. Aliongeza Bw. Msimbano.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali watu Bw. Bernard Marcelline, licha ya kuwapongeza washiriki wa Warsha hiyo, amesema ni imani ya Wizara kuwa warsha hiyo italeta matokeo chanya katika uboreshaji wa Mitaala ya chuo cha Misitu na kukifanya chuo hicho kuendelea kuzalisha wataalam watakao ongeza chachu kwenye uhifadhi na matumizi endelevu ya Misitu nchini.
Mitaala inayoboreshwa ni pamoja na Stashahada ya awali ya Misitu, Astashahada ya Misitu, Stashahada ya Jioinfomatiki ya Usimamizi wa Maliasili na Stashahada ya Usimamizi wa Misitu ya Mjini na Mpango wa Maizingira.