Na Sophia Kingimali.
MGOMBEA nafasi ya Uenyekiti wa Chama cha Allience for Democratic Change (ADC) Hassan Doyo amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo na anatarajia kurudisha fomu Kabla ya Juni 20,2024 pindi atakapokamilisha taratibu za kichama.
Ambapo kwa sasa anasubiri watu wa kuwaidhinisha ili waweze kukidhi matakwa ya katiba na sheria ambazo zinawaongoza katika mipango yao ya kuendesha uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11,2024 jijini Dar es salaam baada ya kuchukua fomu amesema zoezi hilo litakuwa limeisha kwa siku tano kwakuwa ana timu kubwa ya kufanya nayo kazi.
Amesema uwezekano wa kuwa mgombea kwa mujibu wa katiba ya Chama ni mkubwa wa kuwa mgombea wa Uenyekiti wa Taifa.
Aidha Doyo amewaahidi kuwa ataenda katika majukumu ya kisiasa kwenda kusukuma agenda ya kuleta mabadiliko ya kisheria amabazo zina matatizo.
Amesema agenda nyingine anaenda kusukuma maisha bora kwa watanzania kwani hali ya maisha ya wananchi inahitaji msukumo wa kiuongozi madhubuti wa Chama cha kisiasa ili Serikali iliyopo madarakani ione namna bora kuweza kufanya marudio ya Sera yake na watanzania waweze kupata mrejeo wa maisha ambayo ni salama na mazuri.
Amewaahidi wanachama wa ADC anakwenda kufanya siasa nzuri na za kistaarabu na siasa za kwenda kukijenga Chama hicho kuwa Chama mjadala.
“Nawaomba watanzania mniombee na wanachama wa ADC wamfanyie kampeni ili niweze kuwa Mwenyekiti wa Chama hichi ifikapo 20 Juni mwaka huu “amesema
Nae Mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ADC Tanzania bara Scollastica Kahana amemshukuru mgombea wa nafasi ya uenyekiti kwa kumpendekeza kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti hivyo amewaomba wanachama wa Chama hicho kuwapa ushirikiano.