Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo ya Nbs yaliyoandaliwa na IUCN mkoani Tanga
Ofisa Programu Mwandamizi wa IUCN, Wendy Atieno.
Washiriki wa mafunzo wakijadili jambo
Ofisa Programu-Mabadiliko ya Tabia nchi wa IUCN, Christopher Roy, alisema IUCN
Mshiriki wa mafunzo, Mjumbe wa Bodi- Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET)
………………..
NA SIDI MGUMIA, TANGA
Shirika la Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) limetoa mafunzo maalum kwa wadau wa mazingira yenye lengo la kujua kwa kina umuhimu wa uhifadhi wa maeneo ya bahari na namna bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mafunzo hayo ya siku mbili, yaliyofanyika mkoani Tanga hivi karibuni ni sehemu ya Mradi wa Uhifadhi mzuri wa maeneo makubwa ya bahari kwa ajili ya maendeleo endelevu ya watu, hali ya hewa na viumbe (ReSea) unaotekelezwa na shirika la Mission Inclusion (Mi) na IUCN nchini Comoro, Kenya, Madagascar, Msumbiji na Tanzania.
Mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa kustahimili hali ya kijamii na kiuchumi kwa watu wanaoishi katika jamii za pwani na kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Ofisa Programu Mwandamizi wa IUCN, Wendy Atieno alisema kuwa shirika hilo limedhamiria kujikita katika kupaza sauti na kuwajengea uwezo washirika wa ndani na watunga sera kuhusu umuhimu wa kutumia suluhu za asili (Nature based Solutions-NbS) kwa ajili ya kukabiliana na hali ya mazingira ya bahari ili kuunga mkono jitihada za kusawazisha na kuzuia uharibifu wa mazingira kwa ujumla.
“Jukumu letu ni kutoa mafunzo haya ambayo yameundwa kwa ajili ya wadau katika nguzo zote tatu (Sayari ya Bluu, Mazingira ya Bluu na Watu wa Bluu), lengo likiwa ni kuwasaidia wadau kuelewa suluhu zinazotegemea asili kama mbinu muhimu ya kukabiliana na uharibifu wa mfumo wa ikolojia na kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema Atieno
Aliongeza kuwa lengo lingine ni kuelewa jukumu la NbS katika mkakati wa jumla wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuelewa kiwango cha NbS kinachofaa na vigezo maalum ndani ya kiwango kinachohitajika pamoja na kuelewa jinsi ya kujitathmini na NbS.
Kwa mujibu wa IUCN, NbS ni hatua za kulinda, kudhibiti na kurejesha mifumo ya asili na iliyorekebishwa ambayo inashughulikia changamoto za jamii kwa ufanisi na wakati huo huo kunufaisha watu na asili.
Akifafanua kuhusu mafunzo hayo, Ofisa Programu-Mabadiliko ya Tabia nchi wa IUCN, Christopher Roy, alisema IUCN kwa sasa inashughulikia changamoto saba za kijamii ambazo ni kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, kupunguza hatari ya maafa, kudhibiti uharibifu wa mfumo ikolojia na upotevu wa viumbe hai, afya ya binadamu, maendeleo ya kijamii na kiuchumi, usalama wa chakula na usalama wa maji.
Roy alisema mabadiliko ya tabia nchi ni sababu kuu ya opotevu wa bioanuai na mabadiliko ya mfumo wa ikolijia hasa katika maeneo ya Pwani na hiyo ni kutokana na uharibifu wa miti ya mikoko, nyasi bahari na matumbawe, hivyo basi ipo haja ya kuelewa athari zilizopo na kufanya bidii kukabiliana na changamoto hizo.
“Tathimini ya kimataifa inaeleza kuwa tuko katika hatari ya kupotea zaidi ya nusu ya mikoko iliyopo ifikapo mwaka 2050. Kina cha bahari kuongezeka kimekuwa ni moja ya sababu kubwa sana ya uharibifu wa mazingira. Bila suluhu ambazo ni za kiasili, athari za mabadiliko ya tabia nchi, majanga yatakuwa ni makubwa na jamii pia itaathirika zaidi. Lakini tukitumia NbS katika bayoanuai yetu basi tunatarajia kuongezeka kwa huduma za ikolojia kama uzalishaji wa misitu na mikoko ambao utasaidia upunguzaji wa hewa ukaa, kupunguza athari za maafa lakini pia mwanadamu kunufaika na huduma hizo na kuweza kujikimu kiuchumi na kupambana na mabadiliko hayo,” alisema Roy
Kwa upande wake Mshauri wa Uvuvi Mkoa wa Tanga, Issa Khatibu, alisisitiza kuwa maeneo ya mwambao wa Tanga pia yapo katika hatari ya kupanda kwa kina cha bahari hali inayoathiri mfumo ikolojia na maisha ya jamii za pwani. Katika kukabiliana na changamoto hiyo serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza wajibu wake kupitia Mkakati wa Kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi (NCCRS) wa mwaka 2021-2026.
“Tuna kampeni za upandaji miti, uanzishwaji wa hifadhi za misitu kwenye ardhi na bahari, ushirikishwaji wa jamii, kutoa elimu na kushirikiana na washirika wa ndani. Vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa ni kubwa na inahitaji kutumia hatua sahihi na kujitolea, lazima tuendelee kukarabati, kushirikiana na kuchukua hatua kwa usahihi ili kulinda mazingira yetu na kupata mustakabali endelevu kwa watoto wetu na vizazi vijavyo,” alisema Khatibu
Mmoja wa washiriki wa mafunzo, Boniventure Mchomvu ambaye pia ni Meneja Uendeshaji kutoka taasisi ya Climate Action Network-International (CAN) ameeleza kuwa ni vyema NbS izingatiwe, misitu ijirejeshe kwenye hali yake ya asili ili ifyonze hewa ukaa iliyopo kwenye tabaka la ozoni.
Alisisitiza kuwa ardhi imeharibiwa na kusababisha madhara makubwa zaidi kwa kupitia shughuli za kibinadamu kama vile kufyeka mikoko kila siku kwa ajili ya kuni, kutengeneza mshamba ya mpunga, mashamba ya chumvi, kwahiyo suluhu ni kurejea katika njia za asili za kupambana na changamoto za mabadilko iliyopo kwa kuzingatia kuzitunza rasilimali zilipo lakini pia kuwaangalia watu katika jamii husika na namna rasilimali hizo zitakavyowasaidia.
“Kikubwa katika mapambano haya ni tubadilishe namna tunavyofanya shughuli zetu lakini pia tubadilishe tabia zetu ambapo sera na vinginevyo vitabadililka vyenyewe,” alisema Mchomvu
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliandaliwa kwa ufadhili wa Serikali ya Canada na kushirikisha wadau wa mazingira kutoka taasisi mbalimbali kama vile Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingra Tanzania (JET), Shirika la kijamii la “Women Fund Tanzania, Shirika lisilo la kiserikali la Sea Sense, CAN Tanzania, Shirika la UZIKWASA, Blue Allience, Maafisa Uvuvi pamoja na Mtandao wa Jamii za Pwani, Pemba, Unguja na Tanga.