Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Siti Abasi Ali akizungumza na Makadhi wa Mikoa ya Zanzibar katika kikao cha kujadili changamoto za kukabiliana na ongezeko la Talaka na utelekezaji wa Watoto huko Sebleni Wilaya ya Mjini.
………….
Na Fauzia Mussa Maelezo. 10.06.2024.
Idara ya maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inekuasudia kuanzisha kitengo cha usuluhishi katika Mahkama za Kadhi ili kuwapunguzia mrundikano wa kesi zinazohusiana na Wanawake na Watoto.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara hiyo Siti Abasi Ali wakati alipokuwa akizungumza na Makadhi wa Mikoa ya Unguja, kikao ambacho kimefanyika huko Sebleni Wilaya ya Mjini.
Amesema lengo la kuanzisha kitengo hicho ni kuweka mikakati bora na imara ya kutatua kesi hizo kwa uhakika na kuondosha manung’uniko kwa jamii.
Amesema Makadhi hao wanapokea kesi nyingi na wakati mwengine wanalazimika kutoa fat-wa kwa haraka kutokana na wingi wake jambo ambalo linachangia ongezeka la Talaka na kupelekea utelekezaji wa Wanawake na Watoto.
Mbali na hayo, amesema vituo hivyo vitapunguza kesi katika jamii ikiwemo mirathi, migogoro ya ndoa na huduma za watoto.
Kwa upande wake Mratibu wa mapambano ya vitendo vya ukatili na udhalilshaji wa Wanawake na Watoto katika Idara hiyo Omar Haji Omar amesema Tafiti zinaonyesha kuwa, idadi kubwa ya Talaka inasababisha utelekezaji wa Watoto katika jamii.
Hivyo amewataka Vijana kuacha kufunga ndoa kwa kufuata mkumbo na mihemko na badala yake wapate elimu kabla ya kufunga ndoa na kuifanyia kazi.
Amesema talaka ni chanzo cha Watoto kutelekezwa na kuharibika na kuwataka wanandoa kufikiria Watoto wao kabla ya kuachana ili kuwaondoshea usumbufu unaojitokeza.
Nao baadhi ya Makadhi hao, akiwemo Kadhi wa Wilaya ya Mjini Sheikh Ali Juma Machano na Kadhi wa Wilaya ya Magharibi B Sheikh Abubakar Ali mohammed wamesema juhudi za kutoa elimu katika jamii bado zinahitajika ili kuondosha utoaji wa Talaka kiholela.
Aidha Wameishauri Idara hiyo, kuwa na mpango wa kuhakikisha masuala ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa inaanzia katika Madawati ya jinsia katika ngazi ya Shehia pamoja na kuwepo Mikakati madhubuti ya kuzinusuru ndoa kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho