Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava kushoto,akimtua ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Namatunu kata ya Malika Halmashauri ya Mji Masasi Josephine Jabu baada ya uzindua rasmi mradi wa maji katika kijiji cha Namatunu.
………………… Na Mwandishi Wetu,
Masasi
WAKAZI wa kijiji cha Namatunu kata ya Malika Halmashauri ya Mji Masasi mkoani Mtwara,wameondokana na adha ya huduma ya maji safi na salama baada ya Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),kutekeleza mradi wa maji ya bomba uliogharimu Sh.milioni 308,561,431.84.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Masasi Mhandisi Juma Yahaya alisema,mradi huo umejengwa na kampuni ya Bison Engineering Co Ltd chini ya usimamizi wa Ruwasa wilaya ya Mtwara umekamilika kwa asilimia 100 na umeanza kutoa huduma ya maji kwa wakazi wa kijiji hicho wapatao zaidi ya 1,561.
Yahaya amesema hayo jana,wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava.
Kazi zilizotekelezwa ni ujenzi wa nyumba ya mashine,uwekaji wa umeme wa jua,ufungaji wa pampu,ujenzi wa tenki la juu ya mnara wa mita 9 la ujazo wa lita 50,000 kujenga vituo vya kuchotea maji vitano na uwekezaji wa mtandao wa mabomba wenye jumla mita 3,461.
Aidha,ametaja faida za mradi huo ni pamoja na wananchi wa kijiji hicho kupata huduma ya maji safi na salama jirani na makazi yao,jamii kupata muda mwingi wa kufanya shughuli za kilimo na ujasiriamali
Faida nyingine baada ya mradi kukamilika,ni kupungua kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu ambayo yalitokana na jamii kutumia maji yasio safi na salama na kumaliza changamoto ya maji katika Zahanati ya kijiji hicho.
Pia alisema,mradi huo umewaondolea wananchi wa kijiji hicho changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama,kwani awali walikuwa wanapata na kutumia maji kutoka kwenye visima vya asili.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava alisema,mradi huo unakwenda kuondoa na kumaliza kabisa kero ya maji na kuachana na matumizi ya maji ya visima na mito kwa wananchi wa kijiji hicho ambayo hayakuwa safi na salama.
Alisema,Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi katika maeneo yote hapa nchini wakiwemo wa kijiji cha Namatunu.
Alisema,kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan,inakusudia kuwawezesha Watanzania kupata huduma ya maji karibu na makazi yao na kuwataka wananchi kulinda miundombinu ya mradi huo.
Alisema,wananchi walikuwa kwenye mateso makubwa ya kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji kwenye visima vya asili,hali iliyopelekea baadhi ya shughuli za maendeleo kufanyika kwa kusua sua.
Zainabu Namase,ameishukuru serikali kwa kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kila siku kwa ajili ya kwenda kutafuta huduma ya maji kwenye mito na vyanzo vingine vya asili.
“tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia,mradi huu kwetu ni kama Historia kwani miaka mingi hatujawahi kupata wala kuona maji ya bomba katika kijiji chetu,tulikuwa tunakwenda kuyafuata maji mbali na makazi yetu na tukitoka asubuhi tunarudi jioni”alisema.