Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele akimkabidhi kitabu chenye orodha ya majina ya vituo vya kuandikisha wapiga kura nchi nzima kwa Profesa Ibrahim Lipumba Mwenyenyiki wa Chama cha Wananchi CUF.
……………….
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Viongozi wa Vyama vya Siasa wametakiwa kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji na maelekezo ya Tume kuhusu zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Akizungumza leo Juni 7, 2024 wakati akifungua mkutano wa Tume ya Uchaguzi na Vyama vya Siasa uliofanyika kwenye ukumbi wa PSSSF Mwenge jijini Dar es Salaam ambao ulikuwa unajadili uboreshaji wa daftari la kudumu wapiga kura,
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele, amesema kuwa vya siasa vitaruhusiwa kuweka wakala mmoja kwenye kila kituo cha kuandikisha wapiga kura kwenye uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kuzinduliwa Mkoani Kigoma, tarehe 01 Julai, 2024.
Mhe. Jaji Mwambegele amesema kuwa kila chama kitapewa nakala ya orodha ya vituo vyote vya kuandikisha wapiga kura, huku akieleza kuwa lengo ni kuwapatia nakala ili kuwawezesha kupanga na kuweka mawakala wa uandikishaji katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.
Mhe. Jaji Mwambegele amesema kuwa chama kitaruhusiwa kuweka wakala mmoja kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura kwa lengo la kushuhudia utekelezaji wa zoezi la uboreshaji kituoni ikiwemo kuwatambua wale wanaokuja kituoni kama wana sifa za kuandikishwa.
Amesema kuwa mkutano huo ni sehemu ya utamaduni wa tume ya uchaguzi iliojiwekea wa kuwashirikisha wadau wa uchaguzi wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.
“Wadau wanapaswa kuwa pamoja wakiwmo viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu na wanawake” amesema Mhe. Jaji Mwambegele.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Comred Ally Hapi, amesema hatua iliyopo kwa sasa ni muhimu katika ujenzi wa demokrasi katika nchi yetu katika kuwezesha uchaguzi unafanyika.
Ameipongeza tume huru ya uchaguzi kwa kufanya maboresha ya uchaguzi kwa njia ya mtandao na kuleta tija kwa manufaa na kuwawezesha wasimamiziwa uchaguzi kufanya kwa ufanisi.
“Natoa wito kwa viongozi wote wa vyama vya siasa kuhamasisha wanachama wao kwenda kujitokeza katika kuboresha taarifa zao katika daftari la kuduma la wapiga kura, kwani hawataweza kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka kama hawatatekeleza uwajibu huu” amesema Comred Hapi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba ameishukuru tume ya uchaguzi kwa kuwapa utaratibu ikiwemo utekelezaji wa sheria mpya ya uchaguzi.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele akimkabidhi kitabu chenye orodha ya majina ya vituo vya kuandikisha wapiga kura nchi nzima kwa Ali Hapi Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele akimkabidhi kitabu chenye orodha ya majina ya vituo vya kuandikisha wapiga kura nchi nzima kwa Ado Shaibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo.