Katikati ni MKuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akikagua mradi wa kituo Jumuishi cha huduma za Mahakama kinachojengwa eneo la Nanenane Kata ya Msamala Manispaa ya Songea kwa gharama ya shilingi bilioni kumi
SERIKALI imetenga shilingi bilioni kumi kujenga jengo la ghorofa tatu la Kituo Jumuishi cha kutoa huduma za mahakama eneo la Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Mwakilishi wa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo Mhandisi Godfrey Mgwasa amesema mradi huo wa kituo Jumuishi cha mahakama,ukikamilika utakuwa na majengo manne ambayo yatakuwa na mahakama zote na kwamba jengo hilo litakuwa la kisasa lenye lift mbili.
Amelitaja jengo hilo pia litakuwa litatoa huduma kwa watu wote ambao sio watumishi wa mahakama na kwamba jengo hilo pia litakuwa na mashine za kutolea fedha (ATMs) ili kurahisisha huduma kwa wananchi.
Hata hivyo amebainisha kuwa Mkandarasi alikabidhiwa mradi huo Desemba 2023 ambapo mradi unatarajia kukamilika Septemba 2024 na kwamba hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 15,Mhandisi Mgwasa amekiri utekelezaji wa mradi upo nyuma sana.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameyataja madhumuni ya kuanzishwa kwa mradi wa ujenzi wa vituo Jumuishi vya kutoa huduma za za kimahakama katika eneo moja.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa hajafurahishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huo ambapo amemuagiza Mkandarasi kuongeza nguvu kazi na vifaa ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati.
“Ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa mnatakiwa kufanya kazi usiku na mchana kwa kuwa hapa mna kila kitu ukiwemo upatikanaji wa umeme,pia inatakiwa mnunue vifaa vya kutosha zikiwemo kokoto na vifaa vingine ambavyo vinaweza kutumika kwenye ujenzi’’,alisisitiza.
Mwaka 2023 Serikali ilisaini mikataba na kampuni nne yenye thamani ya Shilingi bilioni 49 kwa lengo la kujenga vituo sita jumuishi vya kutoa huduma za mahakama katika mikoa ya Njombe, Katavi, Geita, Simiyu, Ruvuma,na Songwe.