Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Balozi wa Italia anayemaliza muda wake nchini Mhe. Marco Lombardi Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 06 Juni 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimkabidhi zawadi ya picha ya Mlima Kilimanjaro Balozi wa Italia anayemaliza muda wake nchini Mhe. Marco Lombardi mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 06 Juni 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Balozi wa Italia anayemaliza muda wake nchini Mhe. Marco Lombardi mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 06 Juni 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia anayemaliza muda wake nchini Mhe. Marco Lombardi Ikulu Jijini Dar es Salaam aliyefika kwa lengo la kumuaga.
Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amemtakia heri balozi huyo katika majukumu yake mapya nje ya Tanzania na kumpongeza kwa kufanikisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali wakati wa uongozi wake ikiwemo uanzishwaji wa safari za ndege za moja kwa moja kutoka nchini Italia hadi Zanzibar.
Makamu wa Rais amemshukuru Balozi huyo kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa haya mawili katika sekta mbalimbali ikiwemo Uwekezaji, Biashara, Utalii, Afya, Kilimo, Uchukuzi na Utamaduni.
Kwa upande wake Balozi Marco Lombardi amesema ataikumbuka Tanzania ambayo ni kama nyumbani kwa ukarimu na watu wema. Amesema kupita uhusiano mzuri wa Tanzania na Italia katika uongozi wake mafanikio yameonekana ikiwemo kusainia hati za makubaliano katika masuala ya elimu ikiwemo vyuo vya ufundi, uchumi wa buluu, uwezeshaji wanawake na watu wenye ulemavu, ulinzi na uhusiano wa kisiasa.