SHIRIKA la ICAP leo limeikabidhi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC), Maabara ya Kupima usugu wa Dawa za Kufuba za Virusi Vya UKIWMI (VVU),itakayohudumia mikoa minane ikiwemo mitano ya Kanda ya Ziwa.
Mkurugenzi Mkazi wa ICAP nchini, Haruka Maruyama,amesema ICAP kwa msaada wa kiufundi kutoka Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) na ufadhili wa Serikali ya Marekani chini ya Mfuko wa Rais wa Dharura wa Kupambanana UKIMWI (PEPFAR),imekabidhi maabara hiyo BMC.
Amesema kuanzishwa kwa Maabara ya Kupima usugu wa dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI ni hatua muhimu katika kuhakikisha ubora wa huduma za VVU Kanda ya Ziwa na mikoa jirani,hivyo kitakuwa kituo cha kiwango cha juu kitakachohudumia mikoa minane na muhimu katika kudhibiti wa janga la VVU.
“Ushirikiano uliopo umewezesha ICAP kusaidia kwa kiwango kikubwa maabara ya Hospitali ya Bugando kuwa kitovu kikuu cha upimaji na hazina ya Utafiti wa Athari za VVU Tanzania,kwa uwezo wa maabara hiyo upimaji wa uchunguzi wa vinasaba kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na mingine jirani umekuwa na mabadiliko makubwa,”alisema Maruyama.
Amesema maabara hiyo mpya imefikia hatua muhimu ya kuboresha huduma ya matibabu ya Virusi vya UKIMWI na katika mapambano dhidi ya VVU, hivyo ICAP nchini Tanzania, kupitia msaada wa CDC,itaendelea kusaidia BMC na Wizara ya Afya katika afua mbalimbali za afya kwa umma.
Amesema jitihada hizo zimewezesha kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI mkoani Mwanza kutoka asilimia 7.2 mwaka 2016/17 hadi asilimia 4.7 mwaka 2022/23 kwa mujibu wa taarifa ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2022-2023 (THIS 2022-2023).
Mtanda amepongeza jitihada hizo za kuboresha maabara ya kupima usugu wa dawa za kufubaza VVU itakayotumika kusaidia kuboresha huduma za matibabu kwa jamii na watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
Awali Mkurugenzi Mkazi wa CDC nchini,Dr Mahesh Swaminathan alisema miaka zaidi ya 15,PEPFAR kupitia CDC imesaidia BMC na kuimairisha mifumo ya afya ya maabara katika mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar.
“Ushirikiano wetu na Bugando kupitia teknolojia ya hali ya juu imebadilisha maabara hiyo kuwa chombo endelevu kinachojiendesha, kinachotoa huduma za maabara za kiwango cha juu katika mikoa zaidi ya nane na kupanua huduma kwa nchi jirani kama DRC na Burundi.Tangu mwaka 2022, PEPFAR na CDC kupitia ICAP tangu mwaka 2022 zimetoa zaidi ya Dola za Marekani 750,000 (takribani shilingi za Kitanzania bilioni 1.942 kusaidia ujenzi wa maabara ya vinasaba ya BMC iliyoanzishwa kufanya shughuli upimaji,” Dr.Mahesh.
Naye Mkuu wa Mkoa, Dr.Thomas Rutachunzibwa amelishuruku Shirika la ICAP kwa kuendelea kutekeleza mradi wa FIKIA+ wa Afua za UKIMWI,unaotekelezwa katika wilaya saba mkoani humu ili kuimarisha huduma za tiba na matunzo kwa wanaoishi na VVU.
Mkurugenzi wa BMC,Dr.Fabian Massaga amesema maabara hiyo italeta mazingira rafiki kwa wanafunzi na wanasayansi mbalimbali nchini kufanya mafunzo na tafiti zitakazoleta mapinduzi chanya katika huduma za afya na kuomba ushirikiano huo uwe endelevu katika kutoa huduma za afya na matibabu kwa jamii.