Na Sophia Kingimali.
Wananchi wametakiwa kutumia mafundi wenye leseni pindi wanapotandaza waya za umeme ‘wirering’ kwenye nyumba zao lakini pia kufanya marejeo ya mara kwa mara ili kuepuka majanga yanayotokana na itilafu za umeme lakini pia kuvuja kwa umeme kunakopelekea kutumia gharama kubwa ya umeme tofauti na matumizi.
Hayo amesemwa leo juni 5,2024 na Afisa uhusiano huduma kwa wateja TANESCO mkoa wa Kinondoni kaskazini Flaviana Moshi ikiwa ni siku ya pili ya elimu kwa umma inayotolewa na shirikia hilo lengo likiwa kuendelea kuwajengea elimu wananchi kuhusu matumizi sahihi ya umeme.
Amesema changamoto nyingi zinazowakuta watumiaji wa umeme majumbani huwa zinasababishwa na mfumo wa umeme ambao wameweka.
“Majanga mengi ya umeme yanatokana na utandazaji wa umeme unaofanywa na mafundi wasio na taaluma niwashauri wananchi watumie mafundi wenye leseni lakini kukagua mara kwa mara kwenye mifumo yao,maana mifumo hii inapaswa kukaguliwa kila baada ya miaka mitatu mpaka mitano”,Amesema Moshi.
Aidha ameongeza katika kujikinga na uharibifu wa mali unaosababishwa na shoti ya umeme wananchi wanapaswa kutumia vifaa maalumu vya kupunguza nguvu ya umeme ‘Guard’ katika vyombo vyao vya umeme.
“Nipende kuwashauri watumiaji wa vifaa vya umeme kutumia hizi guard kama Tv guard na fridge guard ili kusaidia kupunguza nguvu ya umeme kwenye vyombo hivyo”,Amesema.
Akizungumzia matumizi ya umeme mwingi tofauti na matumizi ya nyumbani amesema tatizo hilo linatokana na kuvuja kwa umeme kutoka kwenye njia yake.
Amesema pindi mwananchi anapopata tatizo hilo wanapswa kulipoti ili ukaguzi ufanyike kwenye njia ya umeme pasipo kupuuzia na kuja kutupia lawama shirika hilo.
Kwa upande wao wananchi wa Mtaa wa Mlalakuwa Mwenge Dar es salaam wamepongeza shirika hilo kwa kuwapa elimu na huduma katika mitaa yao.
Hashimu Juma mkazi wa Mlalakuwa amekiri kutokujua kama anapaswa kukagua ‘wirering’za nyumba yake mara kwa mara na kuahidi kufanya hivyo ili kuepuka majanga yanayotokana na umeme.
Shirika la umeme TANESCO Kinondoni Kaskazini inaendesha elimu kwa umma katika maeneo mbalimbali ya mkoa lakini kuwasogezea wananchi karibu huduma na kuwasaidia kutatua changamoto zinazotokana na umeme.