Na SOPHIA KINGIMALI.
Chama cha Wafanyabiashara wa Ng’ombe Tanzania (TCCS) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) wameandaa maonesho ya Kimataifa ya mifugo yatakayoambatana na mnada yanatarajia kufanyika Juni 14 hadi 16 2024 Wilaya ya Chalinze mkoa wa Pwani yakiwa na kauli mbiu isemayo”Fuga kibiashara tujenge kesho iliyo bora”
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 5 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa TCCS, Naweed Mulla amesema chama hicho kimelenga kukuza kilimo kwa kuandaa maonyesho hayo kila mwaka yanayofahamika kwa jina la “TCCS Livestock Show and Auction”.
“Maonesho haya ni ya siku tatu yatawaleta pamoja wafugaji wa kibiashara, wauzaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa, wafugaji wa mifugo mbalimbali wakulima, wapenzi wa burudani na pamoja na wasambazaji wa pembejeo zingine,”amesema Mulla.
Amesema lengo la maonesho hayo ni kuwawezesha, wafugaji, wasindikaji na wadau wengine nchini kushawishi sera za maendeleo na kukuza uzalishaji wa mifugo endelevu kwa njia kuwajengea uwezo na mitandao.
“Ufugaji endelevu wa uchumi unaoongozwa na kilimo takwimu zinaonyesha sekta ya mifugo inakuza Pato la Taifa kwa asilimia 30 katika nchi zenye kipato cha chini na kati hivyo kaya za vijijini zinategemea mifugo kwa asilimia 60 hadi 80,”amesema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara Mipango na Ushauri na Mahusiano ya Taasisi TADB, Waziri Mkani amesema sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi zimeleta mageuzi katika uchumi.
Amesema kuhakikisha watanzania wanafuga kwa tija na wananufaika na ufugaji na TADB ilitoa mkopo wenye thamani ya shilingi bilioni 38 kwa wafugaji 8,688 kwa mikoa 21.
“Wafugaji wanahitaji kufanya biashara wanahitaji kuwezeshwa hivyo benki ya TADB ipo kwaajili ya kuwawezesha wafugaji watoke kwenye ufugaji wa kawaida uwe wa kibiashara wanufaike,”amesema Mkani.
Aidha amesema TADB imekuwa chagizo kwa taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa wafugaji, kilimo na uvuvi ili kuleta maendeleo katika sekta hizo.
Nae,mwenyekiti wa chama cha wafungaji mkoa wa Pwani Ngobere Msamau amesema kupitia maonesho hayo wamejifunza mambo mengi na kuondokana na kufuga kwa mazoea na kuingia kwenye kufuga kibiashara huku akitoa rai kwa TCCS kuendelea kuwapa elimu ya ufugaji wa kibiashara lakini pia kuangalia namna ya kuwapatia madume ya Ng’ombe ya mbegu bora ya kibiashara ili noa waweze kuingia kwenye biashara ya kimataifa.