Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara yake imepokea maelekezo ya Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi kuhusu suala la ‘Boom’ kwa wanafunzi wa vyuo nchini.
Dkt. Nchimbi akiwa eneo la Usa River jana Juni 04,2024 Wilaya ya Arumeru alitoa maagizo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha wanafunzi wa vyuo wanalipwa fedha hizo ifikapo mwisho wa mwezi June.
Profesa Mkenda ambaye ni mbunge wa Rombo akizungumza kwenye kikao cha ndani cha viongozi na mabalozi wa chama cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, alisema kuwa Wizara yake imepokea agizo hilo na kwamba watalitekeleza kabla ya mwisho wa mwezi.
“Ndugu Katibu Mkuu jana pale Arusha ulitoa maelekezo kuhusu suala la boom na naomba nitumie nafasi hii kusema kuwa suala hilo tutalifanyia kazi na kabla ya muda uliyotoa wanafunzi wote nchini watalipwa” alisema.
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Balozi Nchimbi ameambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Komredi Amos Gabriel Makalla na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Hamid Abdalla.