Josephath Kisamalala – Mrajis msaidizi wa Vyama vya Ushirika vya kifedha akizungumza katika mafunzo hayo mkoani Arusha.
Collins Nyakunga – Naibu Mrajis (Udhibiti na Usimamizi) akiwa katika mafunzo hayo mkoani Arusha .
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo mkoani Arusha .
……….
Happy Lazaro,Arusha.
Warajis wasaidizi na Maafisa Ushirika wametakiwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima inayoweza kutokea katika Vyama vya Akiba na mikopo vilivyopo katika maeneo yao ya kazi.
Hayo yamesemwa na Naibu Mrajis (Udhibiti na Usimamizi) Collins Nyakunga alipokuwa akifunga Mafunzo ya siku tatu (3) kwa Warajis Wasaidizi na Maafisa Ushirika wa mikoa ya Kilimanjaro,Arusha, Mbeya, Mwanza, Kagera,Dodoma na Dar es salaam yaliyofanyika kuanzia Mei 18 hadi 20 Jijini Arusha.
“Sisi kama wasimamizi tuone thamani ya kile tunachojifunza na kwa wale tunaowasimamia ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima, tunafahamu tusipofanya jukumu letu la usimamizi vizuri basi ni dhahiri kwamba hii migogoro haitaisha na tutatumia gharama kubwa sana kusuluhisha migogoro badala ya kufanya majukumu yetu ya usimamizi ili kudhibiti hayo, amesema Nyakunga.
Akitaja malengo ya Mafunzo hayo Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika wa kifedha Josephath Kisamalala amesema ni kuwajengea uwezo Warajis Wasaidizi na Maafisa Ushirika kwenye utekelezaji wa Sheria za huduma ndogo za kifedha, Sheria za Vyama vya Ushirika namba 6 ya mwaka 2013 na miongozo inayotolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika.
Aidha,malengo mengine aliyoyataja ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kusimamia na kuimarisha utendaji wa kazi na kujadilili namna ya kuimarisha utendaji kazi, ukaguzi na usimamizi wa mifumo inayotumika kwenye SACCOS na kuandaa na kukamilisha taarifa ya utendaji wa SACCOS kwa mwaka 2023,amesema Kisamalala.
Aidha Naibu Mrajis amewashukuru wawezeshaji wa mafunzo hayo ambao ni Muungano wa Vyama vya Akiba na Mikopo(SCCULT) na Shirika lisilo la kiserikali linalotoa Elimu ya kifedha (DSIK) kwa ushirikiano mkubwa waliotuoa kwa kuwezesha mafunzo hayo na kuwaomba kuendelea kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika ( TCDC) katika kufanikisha adhima ya Serikali ya kukuza sekta ya Ushirika nchini.