WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu,Dk Dorothy Gwajima na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania, Bi. Isabella Maganga wakiwasili kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam kwa ajili ya Uzinduzi wa Dirisha Maalumu la Kumuwezesha Mwanamke Kukua Kiuchumi lililoandaliwa na Benki ya Equity na kuhudhuriwa na Wanawake zaidi ya 200.
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu,Dk Dorothy Gwajima akizungumza na wanawake wakati wa uzinduzi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania, Bi. Isabella Maganga akimkaribisha Waziri Dkt. Doroth Gwajima ili kuzungumza katika uzinduzi huo
……………………….
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu,Dk Dorothy Gwajima amewataka Wanawake kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa kutanganza biashara zao zaidi na kazi wanazofanya.
Amewaomba wanawake kila kukicha asubuhi kuingia mtandao waangalie fursa kupitia Wizara mbalimbali kwani zitawasaidia kukua kiuchumi.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo Mei 20, 2024 wakati aliposhiriki katika Uzinduzi wa Dirisha Maalumu la Kumuwezesha Mwanamke Kukua Kiuchumi lililoandaliwa na Benki ya Equity na kuhudhuriwa na Wanawake zaidi ya 200 kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.
Amewataka wanawake kuacha kutumia mitandao vibaya kwa kudurusu taarifa za uongo na picha zisizo na maadili kwani hili ni janga kwao na kwa taifa kwa ujumla.
“Ombi langu kwenu wanawake durusuni biashara zenu mpate wateja na kipato kiongezeke,”amesema Dkt. Gwajima.
Amezitaka taasisi za fedha kutokuwasahau wanaume wanapotoa huduma za kifedha hasa mikopo kwani itasaidia kuondoa migogoro ya kifamilia.
“Rai yangu kwa taasisi za fedha mnapotoa mikopo na huduma za kibenki ili kumkomboa mwanamke hakikisheni mnambeba na mwanaume kwani mkimuacha mwanaume ataona kazidiwa kipato na mwisho wa siku itatokea migogoro baina yake na mke wake inayoweza kusababisha vifo na majeraha ya kudumu,”
Alisisitiza:”unapotoa asilimia 50 kwa mwanamke na mwanaume mpe hizo asilimia 50 hii itasaidia wanaume kuishi mda mrefu na kuondoa msongo wa mawazo juu yao na kutengeneza familia yenye amani,”Dk Gwajima.
Sambamba na hilo Dk Gwajima aliwaomba watoa huduma za kibenki kuwafikia Wanawake walioko vijijini kwani wao ndio wanapata changamoto kubwa ya kiuchumi, mwanamke anatafuta alafu mwisho anadhurumiwa haki yake, nijukumu lenu kama watoa huduma kupeleka elimu hii kupitia makongamano,warsha na vyombo vya habari ilikumkomboa mwanamke.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania, Bi. Isabella Maganga, amesema kuwa kuwa mahitaji ya mikopo kwa wanawake katika taasisi za fedha nchini ni shillingi trilioni 4. 4 ambazo bado hazijafikiwa.
Bi. Maganga amesema kuwa kama taasisi za fedha zikifia kiasi cha shillingi trilioni 4. 4 itasaidia kukua kwa uchumi kwa asilimia nne.
Amesema kuwa zaidi ya asilimia 30 ya wanawak bado wana uhitaji mkubwa kutokana na kwamba hawajafikiwa na elimu ya biashara pamoja na huduma za kifedha.
“Kuna wafanyabiashara wanawake ambao wanaongeza thamani bidhaa zao na bado hawajafika kiwango ambacho tunaweza kusema wakizalisha bidhaa kitaingia katika soko na kukubalika katika kiwango ambacho kinakubalika na kuvuka mipaka ya nchi” amesema Bi. Maganga.
Amefafanua kuwa zaidi ya asilimia 54 ya biashara ndogo, kati na kubwa zinamilikiwa na wanawake hivyo wakiendelea kupata fursa watapiga hatua kubwa ya maendeleo.
Bi. Maganga amesema kuwa fursa inayomzunguka mwanamke ni kubwa ambayo inagusa jamii, kushuka kwa riba zote za undeshaji wa biashara ikiwemo gharama za mikopo na uendeshaji wa akaunti itamsaidia kufikia malengo tarajiwa.