NA VICTOR MAKINDA: MOROGORO
Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi zinatokana na uharibifu mkubwa wa mazingira watoto walio katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari wanapaswa kufundishwa kwa vitendo umuhimimu wa utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti na kuitunza.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mazingira na Maendeleo kwa Umma Tanzania, (CWMUT), Elibarick Kweka, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha watoto katika utunzaji wa mazingira, mjini Morogoro jana.
Kweka alisema kuwa wazazi, walezi na walimu wanapaswa kuwajengea watoto hususani walio katika ngazi za elimuya msingi na sekondari tabia za kimazoea za kupenda kutunza mazingira kwa kufundishwa umuhimu wa kupanda miti na kuitunza sambamba na kutunza mazingira kwa ujumla kuepuka matokeo ya athari za uhabifu wa mazingira zinatokea maeneo mengi Duniani.
“Ulimwengu unakabiliwa kwa kiasi kikubwa na matokeo ya uhabifu mkubwa wa mazingira, hivyo jamii inapaswa kuwafundisha na kuwajengea tabia za kimazoea watoto kupanda miti ili kurudisha uoto wa asili uliopotea sambamba na kutunza mazingira kwa ujumla wake.Anasema Kweka.
Kweka anaongeza kuwa CWMUT imejikita katika kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwenye shule shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha wanapata elimu na kuzifahamu mbinu mbali mbali za kutunza na kuhifadhi mazingira ikiwemo kupanda miti shuleni na nyumbani wanakoishi.
Anasema kuwa taasisi ya CWMUT sambamba na miradi mingine ya uhifadhi wa mazingira inayotekeleza, imefanikiwa kuwahamsisha wanafunzi kupanda miti 5000 ya matunda katika shule nne za msingi ndani ya Manispaa ya Morogoro ambayo kwa sasa baaadhi ya miti hiyo imeanza kutoa matunda ambayo wanafunzi hao wanakula wakiwa shuleni.
Naye Anton Mkoba Mwalimu wa mazingira Shule ya Msingi Mwande Manispaa ya Morogoro alisema kuwa kwa msaada wa taasisi ya CWMUT wamepanda miti 200 ya matunda shuleni hapo na wananfunzi wanashirikishwa kikamilifu katika utunzaji wa miti hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Johnson Lazaro, mwanafunzi wa darasa la saba shule ya Msingi Mwande, alisema kuwa wanafunzi wa shule hiyo wamefundishwa umuhimu wa kupanda miti ambapo baadhi yao wamepanda miti hiyo nyumbani kwao.