Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi imefanikiwa kuandikisha wanafunzi 9,449 wa darasa la awali tangu kuanza kwa muhula mpya wa masomo kwa shule za msingi mnamo Januari 8 mwaka 2024 wakiwemo wavulana 4,827 na wasichana 4,622.
Mratibu Idara ya Elimu Msingi katika Manispaa ya Mpanda Victor Rutajumurwa amesema maoteo yalikuwa ni kupata wavulana 3,640 na wasichana 3,707 jumla 7,347 na kuongeza kuwa wanafunzi walioandikishwa ni asilimia 129.
Ameongeza kuwa kumekuwa na ongezeko la uandikishaji mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2023 maoteo yalikuwa wavulana 4,106 na wasichana 4,048 jumla 8,154 lakini waliandikisha wanafunzi wavulana 4,588 na wasichana 4,907 jumla 9,495 sawa na asilimia 116.
Hali hiyo inatokana na uboreshaji wa mazingira ya kusomea ambayo yanamjenga mtoto kisaikolojia na kumweka tayari kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza.
“Ukiangalia katika madarasa mapya ya awali ambayo yamejengwa katika baadhi ya shule utaona maboresho makubwa ukiwepo uzio ambao unasaidia kupunguza utoro na muingiliano kati ya wanafunzi wa madarasa ya juu na darasa la awali, pia unaboresha usalama wa wanafunzi” alisema Rutajumurwa.
Ameongeza kuwa serikali imewekeza katika madarasa hayo ya kisasa ili kukuza umahiri wa wanafunzi na sio kufundisha wanafunzi kwa kuwakaririsha tu.
Amewataka wazazi kutowaacha watoto wazurure hovyo na badala yake wajenge mazoea ya kukagua kazi za shule za watoto wao.
“Wazazi wasiwaachie walimu peke yao, watusaidie kufuatilia maendeleo ya watoto wao” alisema.
Mkuu wa mkoa wa Katavi Bi. Mwanamvua Mrindoko amesema serikali ya awamu ya tano imeboresha miundombinu ya madarasa kwa kipindi cha Januari hadi Disemba 2023 ambapo mkoa huo ulipokea kiasi cha shilingi bilioni 19.4.
Aidha fedha hizo zimeweza kujenga shule mpya kumi za msingi na kuongeza vyumba vya madarasa katika baadhi ya shule zilizokuwa zikikabiliwa na msongamano wa wanafunzi kama shule ya msingi Kasekese iliyokuwa na zaidi ya wanafunzi elfu nne.
Aliongeza kuwa madarasa hayo yameweza kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuwapokea wanafunzi wapya wa madarasa ya awali na darasa la kwanza.
Mkuu huyo wa mkoa wa Katavi ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kuwaandikisha shule watoto wote walio katika umri stahili.
“Elimu ni jambo la msingi sana, ifike mahali kinamama wenzangu msione fahari kukaa na watoto nyumbani. Wapelekeni shule wakachangamane na wenzao. Hata kama una mtoto mlemavu mtoe mpeleke shule hutakuja kujutia maamuzi hayo” alisisitiza Mrindoko.
Shirika lisilo la kiserikali la LARDEO linalotekeleza mradi wa PJT-MMMAM kwa kushirikiana na serikali mkoani Katavi linatambua umuhimu wa wazazi kuandikisha watoto shule.
Mkurugenzi wa Shirika hilo Askofu Ephraim Ntikabuze ameendelea kuhamasisha wazazi wenye watoto wenye umri wa miaka mitano kuwaandikisha shule.
Kwa upande wao baadhi ya watoto walioandikishwa darasa la awali walionyesha furaha ya kuanza shule japo baadhi yao walikuwa wakilalamika kusumbuliwa na njaa.
“Ona leo nimepata zote! Mjomba anaenda kunipa hela ya pipi!” alisema Mariam Kalale mwanafunzi wa darasa la awali katika shule ya msingi Tulieni huku akionesha daftari lake la Hisabati.
“Hakuna chai wala hatuli njaa inauma” alisema Adam Mwakatobe ambaye pia ni mwanafunzi wa shule hiyo hiyo.
Wakizungumzia suala la chakula shuleni baadhi ya wazazi wenye watoto katika shule ya msingi Tulieni wamekiri kukubaliana kuchanga shilingi 5,000/- kwa ajili ya watoto kupikiwa uji.
“Mimi nimeshatoa 10,000/- maana nina watoto wawili wa chekechea lakini wengine hawajachanga” alisema Ibrahim Pesambili mmoja wa wazazi.
Mwalimu Anastazia Makwaya ambaye ni Msimamizi wa darasa la awali katika shule ya msingi Tulieni ameeleza kuwa wazazi wengi hawajatoa mchango wa chakula na kupelekea kushindwa kuwapikia watoto.
“Tunawaruhusu wanafunzi kutoka saa nne asubuhi wanarudi nyumbani mpaka siku inayofuata maana huwezi kuwaweka muda mrefu watoto wakiwa na njaa” alisema mwalimu Anastazia.
Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Katavi bi. Crecensia Joseph ameendelea kusisitiza wazazi kuchangia chakula cha wanafunzi.
Hata hivyo wako wazazi ambao bado hawajatilia mkazo elimu ya awali ambao licha ya kuwaandikisha shule lakini watoto hao wamekuwa hawahudhurii darasani, wengine wakiandikishwa elimu binafsi za jioni (tuition) na wengine wakisafiri na jamaa zao kwenda mikoa tofauti na shule ilipo.
Kwa mujibu wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023; iliyotolewa na wizara ya elimu, sayansi na teknolojia, kifungu namba 2.4. Madhumuni ya elimu na mafunzo kwa kila ngazi ya elimu nchini ni kuwa; Elimu ya Awali inalenga kumwandaa mtoto kimakuzi, kimwili, kiakili, kimaadili, kijamii na kijinsi; kumwezesha mtoto kujitambua mwenyewe na mazingira yanayomzunguka; kubaini mtoto mwenye mahitaji maalumu na kumpa fursa stahiki; kumwezesha mtoto kumudu lugha mbalimbali; na kumwandaa mtoto kujiunga na elimu ya msingi.
Mkoa wa Katavi umevuka lengo kwa kuandikisha jumla ya wanafunzi 52,946 kwa muhula wa masomo mwaka 2024; wa darasa la awali na wanafunzi 47,765 wa darasa la kwanza.
Lengo la mkoa huo lilikuwa ni kuandikisha wanafunzi 42,974 wa darasa la awali na kwa upande wa darasa la kwanza wanafunzi 39,326.
Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki katika elimu ya awali kwa kuifanya kuwa ya lazima kwenye sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014.
Sera hiyo inataka elimu ya msingi kujumuisha elimu ya awali kwa shule zote kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Taifa ya malezi, makuzi na mendeleo ya mtoto ya 2021 kuwepo kwa mazingira rafiki ya kisera kumepelekea ongezeko la uandikishaji wa watoto wa darasa la awali.
Wanafunzi wa darasa la awali nchini wameongezeka kwa asilimia 41.1 kutoka watoto 1,404,998 mwaka 2012 mpaka watoto 2,120,667 mwaka 2016.