JAMII imetakiwa kubadili mitazamo hasi juu ya suala la ushiriki wa wanawake katika michezo mbalimbali ili nao waweze kupata haki yao ya msingi ya kuchangamana kupitia michezo hiyo.
Wito huo umetolewa na mtaalam wa masuala ya kijinsia na mwandishi wa habari mkongwe nchini, Bi Hawra Shamte, akizungumza na waandishi wa habari za jinsia na michezo Zanzibar katika mafunzo ya kuwajengea uwezo kuandika habari za michezo katika mtazamo wa jinsia na ujumuishi kupitia programu ya michezo kwa maendeleo.
Katika mafunzo hayo kisiwani Pemba yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Bi Hawra amesema jamii bado hazitoi nafasi kwa wanawake na wasichana kushiriki katika fursa za michezo kutokana na hofu na mitazamo hasi iliyojengeka jambo linalopelekea kuwakosesha fursa mbalimbali zinazotokana na michezo ikiwemo afya, ajira na kipato.
Alieleza wasichana wengi wanashindwa kufikia ndoto zao kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili katika michezo ambavyo hupelekea wazazi na jamii kuona michezo sio sehemu salama kwa wanawake.
“Bado hakuna idadi sawia ya wanawake wanaopata mamlaka katika tasnia ya michezo, ukatili na ujira mdogo kwa wanawake wanamichezo ni miongoni mwa sababu zinazoshusha hamasa kwa wasichana wengi kujihusisha na michezo.” Hawra alieleza.
Katika hatua nyingine alishauri vyombo vya habari kuweka mkakati wa kuandika kwa kina habari za michezo na jinsia ili kuchochea hamasa na mabadiliko chanya katika jamii juu ya dhana ya michezo kwa maendeleo na ushiriki wa wasichana katika michezo mbalimbali.
Alieleza, “mara nyingi vyombo vya habari hutoa nafasi ndogo katika kuandika habari za wanawake wanamichezo hata pale ambapo mafanikio yao yanapokuwa makubwa kuliko yale ya wanaume.”
Aliongeza kuwa, “wanahabari tuna wajibu wa kuripoti na kuhamasisha wanawake na wasichana kuanzia ngazi ya sikuli ili washiriki katika michezo kwa maendeleo.”
Mapema mratibu wa programu ya michezo kwa maendeleo TAMWA ZNZ, Khairat Haji, aliwataka waandishi kutumia ujuzi wa mbinu za michezo kwa maendeleo kuandika habari chanya dhidi ya wanawake wanamichezo ili kuleta mabadiliko katika jamii na kufikia hatua ya wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika sekta ya hiyo.
Salim Hamad, mwandishi wa habari mtandao wa Pemba post alisema vyombo vya habari vikiweka mkakati maalum wa kuripoti kwa kina umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika michezo utasaidia kukuza usawa katika nyanja mbalimbali.
“Wandishi wa habari tukiandika fursa za wanawake kwenye michezo na wakifanikiwa kuingia katika michezo itasaidia mambo mbalimbali ikiwemo kuimarisha afya, uchumi na kuondosha ubaguzi uliopo wa kuona wanawake hawawezi kushiriki katika michezo,” alieleza Salim Hamad.
Program ya Michezo kwa Maendeleo inatekelezwa na TAMWA ZNZ, ZAFELA na Center for Youth Dialogue kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na shirika la Deutsche Gesellschaft für Internationale Zusammenarbeit (GIZ) la Ujerumani ikiwa na lengo la kuhamasisha waandishi wa habari kuandika habari za michezo na ushiriki wa wanawake katika michezo.