Na Adeladius Makwega-MWANZA
“Roho ya Mungu Imeujuzaaa Ulimwenguuu….Nayo Itaviunganisha Viumbeee vyoteee…”
Hayo yalikuwa maneno ya utangulizi kabisa katika misa hii ya kwanza katika wimbo wa kwanza wa misa iliyoanza saa 12. 00 ya asubuhi,Jumapili ya Mei 19, 2024 iliyoongozwa na Padri Samson Masanja katika Kanisa la Bikira Maria-Malikia wa Wamisionari, Parokia ya Malya-Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.
“Kwa Jina la Baba na La Mwana na Roho Mtakatifu –Aminaa… Bwana awe nanyiii… Awe Rohoni Mwako. Wakristo Wapendwa karibuni katika adhimisho la Misa Takatifu, leo hii tunaadhimisha Dominika ya PENTEKOSTI, dominika ambayo tunaadhimisha Mwanzo wa Kanisa, Kuzaliwa kwa Kanisa, ni siku hamsini zimetimia tangu tulipoadhimisha ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Katika dominika hii ya leo Roho Mtakatifu ndiyo anawatokea Mitume, na wao wanaanza kazi ya Uinjilishaji, kwa kuitangaza Injili ya Kristo kwa lugha mbalimbali. Nasi tuliobatizwa tunampokea huyu huyu Roho Mtakatifu,tunakuwa washirika pamoja nao katika kumuhubiri Kristo.”
Katika misa hii mara baada ya kusomwa Somo la Pili ilisomwa Injili na Padri Masanja mwenyewe na haya yalikuwa maneno ya mwisho mwisho.
“Naye alipokwisha kusema hayo akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi walifurahi walipomuona BWANA,basi Yesu akawaambia tena, ‘AMANI IWE KWENU,KAMA BABA ALIVYONITUMA MIMI, MIMI NAMI NAWAEPELEKA NINYI.’
Basi alipokwisha kusema akawavuvia na kuwaambia,
‘POKEENI RoHO MTAKATIFU WOWOTE MTAKAOWAFUNGULIA DHAMBI WAMEFUNGULIWA NA WOWOTE MTAKAOWAFUNGIA DHAMBI WAMEFUNGIWA.’
Neno la BWANA-Sifa kwako eeh Kristo.”
Wakati wa mahubiri ya misa hii Katekista Antony ndiye aliyesimama katika marufaa ya Kanisa la Bikira Maria Malikia wa Wamisionari na kuwaongoza waamini wenzake katika tafakari ya masomo ya dominika ya PENTEKOSTI.
“Mimi na wewe tunaalikwa kuzungumza lugha ya upendo, maisha yetu yawe upendo, matendo yetu yawe upendo, ili Kristo aweze kujulikana kwa watu wote; inawezekana mimi na wewe hatuwezi kwenda kuitangaza Injili kwa watu wengine lakini katika jamii zetu, maisha yetu tunaweza kumtangaza Kristo hasa kwa mwenendo na maisha yetu yasema kile tunachokiamini na matendo yaetu yaseme kile tunachokifuata.”
Misa hii pia iliambatana na nia na maombi kadhaa,
“Utujalie nguvu ya Roho Mtakatifu,ili ituongoze katika njia za maisha yetu Eee Bwana –Twakuomba Utusikie.”
Kwa hakika hadi misa hiyo inamalizika hali ya hewa ya Malya na viunga vyake vyote jua ni la kadili huku hali ya chanikiwiti sasa ikianza kupotea kidogo kidogo, majani yakibadilika rangi kwa kasi, nayo mvua ikiwa tayari imeshaunyanyua mkono wa kwaheri.
Neema ikibaki kwa wakulima wa mpunga mabaweni wakivuna masuke ya mipunga yao.