Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki Sophia Mziray (wakwanza kushoto) akikabidhi boksi lenye dawa mbalimbali kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda (katikati) kulia ni Mkuu wa magereza Mkoa wa Mwanza Justin Kaziulaya.
Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki Sophia Mziray (katika) akizungumza kwenye hafla fupi ya utoaji wa msaada wa dawa katika zahanati ya Gereza kuu la Butimba Jijini Mwanza
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza Justin Kaziulaya, akizungumza kwenye hafla fupi ya utoaji wa msaada wa dawa ambapo amesema dawa hizo zitasambazwa kwenye zahanati zote za magereza mkoani humo .
……….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki imetoa msaada wa dawa za kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu zenye thamani ya zaidi ya sh56 milioni katika Zahanati ya Gereza Kuu la Butimba Jijini Mwanza.
Akikabidhi dawa hizo Mei 17, 2024 Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Sophia Mziray amesema dawa hizo zitasaidia kurejesha afya za watu walioshikiliwa kwenye magereza yote yaliyopo Mkoani hapa huku akieleza kuwa mwaka 2022 na 2023 walitoa msaada wa dawa zenye thamani ya sh58 milioni.
“TMDA inatambua uhitaji mkubwa kwenye Magereza na ndio maana tumekuwa tukitoa msaada wa dawa mara kwa mara ili ndugu zetu walioshikiliwa wawe na uhakika wa kupata huduma bora za afya”, amesema Mziray
Aidha, amesema TMDA imekuwa na utaratibu wa kutoa msaada wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ambavyo imekuwa ikiviondoa sokoni baada ya kuzifanyia uchunguzi na kujiridhisha kuwa ni bora,salama na zenye ufanisi na zile ambazo hazina ubora wanaziteketeza kwa utaratibu maalumu kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo NEMC.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, Justin Kaziulaya amesema dawa hizo zitasambazwa kwenye Zahanati zote za magereza mkoani humo ikiwemo gereza la Magu,Ukerewe,Ngudu Wilayani Kwimba,Kasungamile Wilayani Sengerema na Butimba.
Amesema msaada huo siyo tu kwa askari,mahabusu na wafungwa bali utawasaidia pia wakazi wa maeneo jirani pindi watakapofika kwenye Zahanati zilizoko kwenye magereza hayo.
Kwaupande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Gereza Kuu la Butimba, Paschal Shiwala amesema kwa siku wanapokea wagonjwa zaidi ya 60 kutoka nje huku mahabusu na wafungwa wakiwa zaidi ya 100 hivyo msaada huo utasaidia kupunguza adha ya wagonjwa kukosa dawa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ametoa rai kwa wafanyabiashara wa dawa,vifaa tiba na vitendanishi kuendelea kufanya biashara kwa kufuata sheria na taratibu za nchi hatua itakayosaidia kuepuka kuingiza dawa ambazo hazijafanyiwa ukaguzi na kuthibitishwa ubora wake.
Mtanda amewashukuru TMDA kwanamna wanavyojitoa kuwasaidia wafungwa huku akiziomba taasisi nyingine kuiga mfano mzuri wa TMDA wa kuwakumbuka watu walioshikiliwa kwenye magereza na wenye mahitaji mbalimbali.