NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Mamia ya wananchi wa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani pamoja na maeneo mengine ya jirani leo wamejitokeza kwa wingi kwa ajili kutoa heshima zao za mwisho pamoja na kumzika katika nyumba yake ya milele kwa aliyekuwa Diwani wa viti maalumu wa chama cha mapinduzi (CCM) katika halmashauri ya mji Kibaha mhe.Dorice Michael.
Mazishi hayo ambayo yamefanyika nyumbani kwa wazazi wa marehemu huyo eneo la Visiga Madafu Wilaya ya Kibaha yamehudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo viongozi wa chama,serikali,viongozi wa dini pamoja na wananchi.
Viongozi ambao wamehudhuria katika mazishi hayo ni pamoja na Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Mama Selina Koka,Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha mji Mwalimu Mwajuma Nyamka, pamoja na viongozi mbali mbali wa jumuiya zote za chama kuanzia ngazi chini ikiwemo za Wilaya na Mkoa.
Pia katika msiba huo viongozi mbali mbali wa serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon pamoja viongozi wengine wakiwemo wakuu wa idara na viongozi mbali mbali.
Akitoa salamu za rambi rambi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Kibaha Katibu Method Mselewa amewapa pole wafiwa wote familia ya marehemu pamoja na ndugu jamaa na marafiki ambao wameondokewa na mpendwa wao.
Mselewa alisema kwamba Mhe.Mbunge alipaswa kujumuika katika mazishi hayo lakini ameshindwa kuhudhuria kutokana na kupata dharura ambazo zipo nje ya uwezo ikiwemo kuuguliwa na mzee wake.
Naye Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Selina Koka alisema amesikitishwa sana kifo cha diwani huyo ambaye alikuwa ni mchapa kazi hodari hivyo ameacha pengo kubwa katika chama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha mji Mwajuma Nyamka alisema chama kimepoteza mtu muhimu sa na kutokana na diwani huyo alikuwa mcheshi na anashirikiana na viongozi mbali mbali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mussa Ndomba ambaye ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Kibaha mji alisema kwamba katika baraza la madiwani wamepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kuyafanyia kazi yale ambayo amekuwa akijifunza.
Diwani wa kata ya Visiga Kambi Legeza wakati akitoa salamu zake za rambi rambi alimuelezea marehemu Dorice alikuwa ni kiungo kikubwa sana katika kusaidia jamii na kutatua changamoto zao mbali mbali zinazowakabili.
Nao baadhi ya viongozi wa dini hawakusita kumwelezea marehemu Dorisi kwa jinsi alivyokuwa mstari wa mbele katika kumcha Mungu ikiwa sambamba na kushirikiana na viongozi wa dini katika ngazi mbali mbali.
Kuhusiana na taasisi mbali mbali ambazo marehemu alishafanya nazo kazi kwa pamoja walisema wameguswa na msiba huo kutokana na marehemu aliweza kuwapambania kwa hali na mali kuweza kupata fedha ambazo zinatolewa na halmashauri.
Katika msiba huo ambao umeweza kugusa na kuumiza mioyo ya mamia ya wansnchi na viongozi kutoka maeneo mbali mbali ya Wilaya Kibaha mkoani Pwani na maeneo ya jirani ya Jiji la Dar es Salaam.
Marehemu Dorice ambaye alizaliwa mwaka 1980 mpaka kifo chake ameacha watoto wawili na alikuwa ni diwani wa viti maalumu kupitia tiketi ya CCM katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mjini ambapo ameacha alama kubwa kutokana na uchapakazi wake.