Na Mwandishi wetu, Mirerani
NYANZA Group wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametoa msaada kwa watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu.
Mwenyekiti wa Nyanza Group, Malimi Kija amesema wametoa msaada huo kupitia kituo cha Light In Africa kilichopo mji mdogo wa Mirerani, wanaowalea watoto hao yatima na wenye kuishi kwenye mazingira magumu.
Kija amesema kikundi hicho kimenunua vyakula, sabuni, mafuta na taulo za kike, kwa ajili ya watoto hao yatima na wenye kuishi katika mazingira magumu.
Amesema kikundi chao kina utaratibu wa kusaidia jamii kwa kile wanachokipata kupitia shughuli na kazi zao wanazozifanya kwa ajili ya vipato vyao.
“Fedha za kununua mahitaji yote haya wanachama wa Nyanza Group wamejitolea mifukoni mwao siyo kwenye mfuko wetu ni pale tulioguswa na kujitolea,” amesema Kija.
Amesema pamoja na kutoa vyakula hivyo wana Nyanza Group pia wametoa fedha kwa ajili ya kununua maziwa ya kunywa asubuhi pamoja na chai.
Mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani (TEO) Isack Mgaya amewapongeza wana Nyanza Group kwa majitoleo yao na kusaidia watoto hao yatima na waliokuwa wanaishi kwenye mazingira magumu.
Mgaya amesema kitendo kilichofanywa na wana Nyanza Group kinapaswa kuigwa na wana vikundi wengine wa mji mdogo wa Mirerani katika kusaidia wahitaji.
“Misaada hii itumike ipasavyo kwa lengo lililokusudiwa na wana Nyanza Group ambao wamefanya jambo zuri la heri,” amesema Mgaya.
Mmoja kati ya walezi wa kituo cha Light In Africa Mariam Mkali amewashukuru wana Nyanza Group kwa kutoa msaada kwa watoto hao yatima na waliokuwa wanaishi kwenye mazingira magumu.
“Tunamshukuru Mungu kwa neema yake kwani watoto hawa wamekuwa marafiki kwetu na tunawasaidia kwa moyo mmoja, tunawapongeza nanyi kwa kuja kuwasalimia watoto hawa,” amesema Mkali.