Naibu Katibu Mkuu wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Jasson Rwezimula akizungumza katika uzinduzi huo mkoani Arusha
Mkurugenzi Idara ya Sayansi na Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Ladslaus Mnyone akizungumza katika uzinduzi huo.
………..
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Naibu Katibu Mkuu wizara ya elimu sayansi na teknolojia Dkt. Franklin Jasson Rwezimula amezindua mafunzo na awamu ya kwanza ya uanzishaji wa madawati na majukwaa ya Sayansi ,teknolojia,na ubunifu (STU) katika ngazi ya Halmashauri na Majukwaa katika ngazi ya Shule za Msingi na Sekondari, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.
Aidha hafla hiyo ambao imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya nguvu za Atomu Tanzania mkoani Arusha umewakutanisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo maafisa elimu kata,maafisa maendeleo ya jamii na wadhibiti ubora kutoka halmashauri ya Meru,Arusha dc na jiji la Arusha .
Dkt .Rwezimula amesema kuwa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) pamoja masuala mengine, ina jukumu la kutunga na kusimamia utekelezaji wa Sera, Miongozo, Taratibu, Mipango na Mikakati mbalimbali inayolenga kuendeleza na kuimarisha mchango wa Sayansina Ubunifu (STU) katika ujenzi wa uchumi imara na endelevu.
Amesema kuwa, STU ni nyenzo muhimu katika kuongeza tija na kuharakisha ukuaji wa sekta zote za uzalishaji ikiwemo Elimu, Afya, Kilimo, Mifugo, Nishati, Maji, Madini na kutokana na umuhimu huo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuendelea kuboresha mazingira kwa lengo la kuchochea mchango wa STU nchini.
Aidha amesema kuwa ,ili kuchagiza maendeleo na mchango wa STU nchini, Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza afua na mikakati mbalimbali ikiwemo, kutenga fedha na rasilimali nyingine kwa ajili ya kuendeleza na kubiasharisha bunifu na teknolojia zinazoibuliwa nchini kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) na njia nyingine.
“Serikali inaendeleza bunifu 283 zilizobuniwa na watanzania na bunifu 42 kati ya hizo zimeshaingia sokoni,ambapo imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya uanzishwaji wa Vituo vya Ubunifu ambapo hadi sasa kuna vituo takribani 75 nchini’amesema.
Amesema kuwa,imeanzisha vituo vya umahiri vya utafiti na ubunifu ambapo hadi sasa Tanzania ina takribani vituo vya umahiri 12 katika nyanja mbalimbali ikiwemo Kilimo, Mifugo, Afya, Nishati, Usafirishaji na TEHAMA na Serikali inahamasisha vituo hivyo kuiunga mkono katika kuibua na kuboresha bunifu na teknolojia zinazozalishwa na wabunifu na wagunduzi waliopo katika ngazi mbalimbali ikiwemo sekta isiyo rasmi.
Hata hivyo imeanzisha kongano 21 ambazo zinatoa fursa kwa wajasiriamali na wabunifu katika nyanja zinazoshabihiana kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika matumizi ya miundombinu na vifaa vilivyopo.
“Pamoja na mafanikio yaliyoainishwa na mengine, Serikali inaendelea kubuni na kutekeleza afua na mikakati mipya kwa lengo la kuimarisha maendeleo na mchango wa STU nchini. Moja ya mikakati hiyo ni uanzishaji wa Madawati ya STU katika ngazi ya Halmshauri; na Majukwaa katika Shule za Msingi na Sekondari, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Uanzishaji wa Madawati na Majukwaa haya unalenga kuimarisha mfumo wa uratibu na usimamizi wa shughuli za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika ngazi zote nchini ikiwemo mamlaka ya serikali za mtaa. “amesema .
“Mafunzo haya yatafuatiwa na awamu ya kwanza ya uanzishaji wa Madawati na Majukwaa katika mikoa tajwa.na mafunzo haya yatawasaidia kuratibu na kusimamia uanzishaji wa Madawati katika Halmashauri/Wilaya pamoja na Majukwaa katika Shule za Msingi na Sekondari, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Mafunzo kama haya yakifuatiwa na uanzishaji wa Madawati na Majukwaa yataendelea kufanyika katika mikoa mingine kwa awamu kwa kuzingatia uwezo wa kibajeti.”
Amesema kuwa, uanzishaji na uendeshaji wa Madawati na Majukwaa ya STU nchini unatarajiwa kuwa na manufaa mengi ikiwemo,kuimarika kwa mfumo wa uratibu wa shughuli za sayansi, teknolojia na ubunifu kuanzia ngazi za chini , kuimarika kwa uelewa na ushiriki wa jamii katika kuendeleza na kutumia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.
Ameongeza kuwa ,kuongezeka kwa idadi ya wabunifu pamoja na bunifu na teknolojia zinazobuniwa, kutambuliwa, kuendelezwa na kubiasharishwa,idadi ya wabunifu na wagunduzi wenye uelewa wa kutosha juu ya fursa zilizopo na namna ya kulinda bunifu na teknolojia itaongezeka,madawati na majukwaa ya STU yataimarisha mawasiliano baina ya Wabunifu, Taasisi za Elimu ya Juu, Taasisi za Utafiti na Maendeleo na Vituo vya Ubunifu katika ngazi mbalimbali nchini.
“madawati na majukwaa yatafanya masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu kuwa ajenda ya kudumu katika mipango na mikakati katika ngazi mbalimbali kuanzia Halmashauri/Wilaya, Shule za Msingi na Sekondari, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi,na yatachagiza utafiti na ubunifu unaofanywa kwa kuzingatia changamoto na mahitaji ya jamii katika eneo husika; n.k.
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Sayansi na Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Ladslaus Mnyone, amesema kuwa lengo la uzinduzi wa
madawati na Majukwaa ni kuhakikisha kuwa wanaendelea kuimarisha usimamizi na uhamasishaji wa maswala ya Sayansi na Teknolojia na Ubunifu,kwa kuwa maswala haya ni sehemu ya maisha ya Kila siku.
“Kwahiyo washiriki nataka muelewe kuwa tunawategemea kuwa mtatusaidia Kwa kuwa tunataka tuimarishe mfumo wa uratibu na usimamizi wa maswala ya Sayansi na Teknolojia na Ubunifu”amesema Prof.Mnyone .
Naye Suzana Nusu ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu kutoka TAMISEMI amesema kuwa masuala ya Ubunifu yanaanzia ngazi ya kaya katika mitaa mbalimbali ambayo Wizara hiyo inasimamia.
Pia alitumia fursa hiyo Kuipongeza Wizara ya Elimu Kwa kuwashirikisha Maafisa Elimu kata Kwa kuwa kundi Hilo ni muhimu na linaanzia ngazi ya chini kabisa Kwa kuratibu masuala ya Teknolojia na Ubunifu katika shule za Msingi na Sekondari.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyika katika mikoa mitatu ikiwa ni pamoja na Dar es salaam,Arusha na Tanga yakiwashirikisha Maafisa Elimu wa Kata,Maafisa Maendeleo ya Jamii,na Wathibiti Ubora.