Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, akizungumza jambo wakati akifungua Kongamano la Wadau wa Mitandao ya Kijamii ambalo limeandaliwa na Wizara ya Fedha, katika ukumbi wa mikutano wa Nane Nane, mkoani Morogoro kwa siku mbili kuanzia 13 hadi 14 Mei 2024, ambapo wadau hao watapata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali kuhusu Wizara hiyo, na kujengewa uwezo kwenye masuala ya Bajeti Kuu ya Serikali, Mirathi na Pensheni.
Mwenyekiti wa Kongamano la Wadau wa Mitandao ya Kijamii ambalo limeandaliwa na Wizara ya Fedha, Bw. Mathias Canal, akizungumza wakati wa kongamano hilo ambalo limekutanisha wadau hao katika ukumbi wa mikutano wa Nane Nane, mkoani Morogoro kwa siku mbili kuanzia 13 hadi 14 Mei 2024, ambapo watapata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali kuhusu Wizara hiyo, na kujengewa uwezo kwenye masuala ya Bajeti Kuu ya Serikali, Mirathi na Pensheni.
Mhasibu Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, CPA. Jenipha Ntangeki, akizungumza kuhusu Masuala ya Mafao na Pensheni wakati wa Kongamano la Wadau wa Mitandao ya Kijamii ambalo limeandaliwa na Wizara ya Fedha, katika ukumbi wa mikutano wa Nane Nane, mkoani Morogoro kwa siku mbili kuanzia 13 hadi 14 Mei 2024.
Baadhi ya Wadau wa Mitandao ya Kijamii wakifuatilia kwa umakini mada iliyokuwa inatolewa na Mhasibu Mwandamizi kutoka Wizara ya Fedha, CPA Jenipha Ntangeki (Hayupo pichani) kuhusu Masuala ya Mafao na Pensheni wakati wa Kongamano la Wadau wa Mitandao ya Kijamii ambalo limeandaliwa na Wizara ya Fedha, katika ukumbi wa mikutano wa Nane Nane, mkoani Morogoro kwa siku mbili kuanzia 13 hadi 14 Mei 2024.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja (katikati alieketi), Mwenyekiti wa Kongamano la Wadau wa Mitandao ya Kijamii ambalo limeandaliwa na Wizara ya Fedha, Bw. Mathias Canal (Kushoto alieketi) na Katibu wa Kongamano hilo, Bi. Tumaini Silas (kulia aliyeketi), wakiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Mitandao ya Kijamii baada ya kumalizika kwa hafla ya ufunguzi wa Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Wizara ya Fedha, katika ukumbi wa mikutano wa Nane Nane, mkoani Morogoro kwa siku mbili kuanzia 13 hadi 14 Mei 2024.
……………….,
Na Asia Singano na Chedaiwe Msuya – WF – Morogoro
Wizara ya Fedha imeendelea kuwakumbusha wastaafu wanaolipwa mafao na Wizara ya Fedha kutojihusisha na utoaji wa fedha kwa mtu, kama kigezo cha kusaidiwa kupata mafao yao, Kwakuwa huduma hiyo hutolewa bure.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ambaye pia ni Msemaji wa Wizara ya Fedha Bw. Benny Mwaipaja, wakati akifungua kongamano la Elimu kwa Wamiliki wa Mitandao ya Kijamii nchini liliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa NaneNane mjini Morogoro.
‘’Naomba muwataarifu wastaafu na familia zao hususani wale wanaolipwa na Hazina kuwa Wizara ya Fedha hailipishi gharama zozote kwa mstaafu ili kumlipa mafao yake’’ alisema Bw. Mwaipaja.
Akizungumzia kuhusu utoaji wa taarifa za Bajeti Kuu ya Serikali inayotarajiwa kuwasilishwa Bungeni hivi karibuni, Be. Mwaipaja alisema kuwa wadau hao wa mitandao ya kijamii wana fursa kubwa ya kuelimisha wananchi kuhusu maudhui na nia ya Serikali ya kuwaletea Maendeleo.
Aliongeza kuwa wanahabari wana jukumu la kutoa taarifa kwa usahihi ili kuepusha upotoshaji wa taarifa.
‘’Jukumu lenu ni kupeleka ujumbe kwa jamii ambao ni sahihi na wakuaminika, tunahitaji muwaelimishe wananchi kuhusu umuhimu wa kukusanya fedha kwa ajili ya bajeti kuu ya Serikali, kuhamasisha watu kuchangia kwenye bajeti ili kuimarisha na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo’’ alisema Bw. Mwaipaja.
Kwa upande wake Mhasibu Mwandamizi, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Kitengo cha Pensheni CPA Jenipha Josephat Ntangeki alisema kuwa huduma za mafao ya wastaafu wanaolipwa na Wizara ya Fedha ama HAZINA zinatolewa bure na kuwaasa wastaafu kujiepusha na matapeli wanaowarubuni wawapatie fedha ili wawasaidie kupata mafao yao haraka.
Alisema pia kuwa katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali inaunda mfumo wa kidigitali “wastaafu portal” ambapo mstaafu atapata taarifa zake zote kupitia mtandao na wastaafu wataweza kujihakiki kidigitali’’ alisema CPA Ntangeki.
Aliongeza kuwa Wizara ya Fedha inaendelea kutoa elimu kwa Wastaafu na Wastaafu watarajiwa kwa kuwa kustaafu kunaweza kutokea hata kabla ya miaka husika kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto ya kiafya hivyo ni vyema watumishi wa Umma kujiandaa kwa ajili ya maisha yao baada ya kustaafu.
‘’Kwani Kustaafu ni ghafla? Kustaafu maana yake ni kushindwa kupata kile kipato ambacho umekuwa ukikipata siku zote’’ alisema CPA Ntangeki
Akizungumza kwa niaba ya Washiriki wa kongamano hilo hususani Wamiliki na Watendaji Wakuu wa Mitandao ya Kijamii, Mwenyekiti wa Waandishi wa Mitandao ya Kijamii wanaoandika habari za Wizara ya Fedha, Bw. Mathias Canal aliipongeza Wizara ya Fedha kwa mafunzo yanayotolewa kwenye kongamano hilo kwakuwa yanasaidia kuwaimarisha wanahabari katika tasnia yao.
‘’ Leo tunajifunza mambo mawili matatu naamini baada ya kumaliza hapa tutakuwa tumefahamu Sera, Mipango na Mikakati ya Wizara ya Fedha na itakuwa imeturahisishia sisi namna ya kuripoti habari zinazohusu masuala ya Fedha, mafao na mirathi’’ alisema Bw. Kanal.
Hii ni mara ya pili kwa Wizara ya Fedha kufanya Kongamano la Elimu kwa wamiliki wa mitandao ya kijamii hapa nchini.