Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali bungeni jijini Dodoma katika Kikao cha 24 Mkutano wa 15 wa Bunge jijini Didoma leo tarehe 13 Mei, 2024
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwa na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika Kikao cha 24 Mkutano wa 15 wa Bunge jijini Didoma leo tarehe 13 Mei, 2024. Nyuma ni Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa.
………………….
Serikali inaangalia namna ya kupunguza gharama za uingizaji wa vifaa vya nishati safi ya kupikia ili kuwawezesha wananchi kumudu matumizi ya nishati hiyo ikiwemo ya gesi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema hayo bungeni leo tarehe 13 Mei, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Santiel Kirumba aliyeuliza Serikali imejipangaje kuweka ruzuku katika nishati ya gesi ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Mhe. Khamis amesema kuwa ili kuhakikisha hatua hiyo, Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Nishati na Wizara ya Fedha zimekutana na kujadili kuona namna ya kuwasaidia wananchi kutumia kuweza kutumia nishati safi na kuacha kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Pamoja na hayo amesema Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia umependekeza kuwa Wizara zinazohusika zichukue hatua ya kuona namna ya kupunguza gharama hizo ili wananchi wazimudu.
Akijibu swali la Mbunge wa Kalenga Mhe. Jackson Kiswaga aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kupanda miti kando ya mito na barabara, Naibu Waziri Khamis amesema tayari Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wizara na taasisi mbalimbali inaendelea na mpango wa kupanda hususan mkoani Dodoma ili kurejesha miti yaa asili ili kutunza na kuhifadhi mazingira.
Awali katika swali la msingi la Mhe. Kirumba aliyeuliza Serikali imejipangaje kuhimiza wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji miti, Naibu Waziri Khamis amesema katika mwaka 2024/2025, Serikali imepanga kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa utunzaji, hifadhi na usimamizi wa mazingirakwa njia mbalimbali ikiwemo.
Amesema vipindi vya redio na runinga, magazeti, hotuba za viongozi, machapisho ya Ofisi ya Makamu wa Rais na mitandao ya kijamii ni miongoni mwa shughuli za uelimishaji zitafanyika.
Halikadhalika, amesema elimu ya utunzaji wa mazingaira itaendelea kutolewa kupitia maadhimisho mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa ikiwemo Siku ya Wakulima (Nanenane), Siku ya Mazingira Duniani, Siku ya Ozoni Duniani, Siku ya Jangwa na Ukame Duniani,na Siku ya Misitu.
Kwa upande mwingine amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira 2022 – 2032 ambapo pamoja na mambo mengine itaendelea kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti nchini hususani katika Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Kigoma na Katavi.