Na Mwandishi wetu, Simanjiro
Wakazi wa Kata ya Ngorika wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamekumbwa na wakati mgumu baada ya kukumbwa na mafuriko yaliyotokana na mvua hivyo kuhitaji kivuko au daraja.
Wakazi hao hasa wa kijiji cha Nyumba ya Mungu hivi sasa wanatumia mtumbwi kuvuka eneo moja kwenda jingine kutokana na maji ya mafuriko kuzunguka maeneo yao.
Diwani wa Ngorika, Albert Msole akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro amesema wakazi wa eneo hilo wanapaswa kupatiwa msaada.
Msole amesema bwawa la Nyumba ya Mungu lililotengenezwa mwaka 1964 hadi mwaka 1968 kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya umeme limejaa mno na kutapika.
“Tunahitaji kivuko au daraja kwani hali ni mbaya bwawa limejaa mno, linapokea maporomo ya maji kutoka ziwa jipe, Kilimanjaro, mto Kikuletwa na bwawa la kidawashi,” amesema Msole.
Amesema hivi karibuni kuna mfugaji alizama ndani ya bwawa la Nyumba ya Nyumba, akiwa na ng’ombe wake walipokuwa wamepanda mtumbwi na hadi hivi sasa hajaonekana alipo.
“Mfugaji huyo hakuonekana hii ni siku ya nane ila ng’ombe alikufa maji baada ya mtumbwi waliokuwa wameupanda kupasuka na kuingiza maji,” amesema Msole.
Amesema hata boti ya halmashauri hiyo mashine imeharibika hivyo wananchi wa eneo hilo kuwa na wakati mgumu katika kufanya shughuli zao za kiuchumi za kila siku.
“Hali ya uchumi ni mbaya tunahitaji kivuko au daraja ili kuweza kuvuka kutoka sehemu moja au nyingine kwani hata walimu wanapanda mtumbwi ili wafike shuleni,” amesema.
Amesema awali hali hiyo ilikuwa inajitokeza kila baada ya miaka mitano au 10 ila kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, hivi sasa kila baada ya mwaka mafuriko hayo hutokea.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amesema inahitajika viongozi wa wilaya kufika mara moja eneo hilo ili kujionea hali halisi ilivyo.
“Inabidi mimi, mkurugenzi wa halmashauri, kiongozi wa Tarura na diwani wa kata twende tukajionee hali halisi ili tuone namna ya kuwasaidia hao watu,” amesema Kanunga.