NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka amewataka viongozi wa chama kuhakikisha wanaweka misingi ya kuwaheshimu viongozi wote waliopo madarakani na kuachana kabisa na tabia ya kutengeneza safu mpya ya viongozi wapya kabla ya muda kufika.
Mwalimu Nyamka ameyasema hayo wakati wa kikao kazi ambacho kiliweza kuwakutanisha Wenyeviti pamoja na makatibu wote wa CCM ngazi ya Kata kutoka kata zote 14 za Halmashauri ya Kibaha mji lengo ikiwa kujadili mambo mbali mbali ikiwemo kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.
Alisema kwamba viongozi wq chama wanapaswa kuwapa ushirikiano wa kutosha viongozi wote waliopo madarakani kuanzia ngazi za chini hadi za juu ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo bila ya kusumbuliwa kwani bado wapo madarakani.
“Tumekutana katika kikao kazi hiki na nimewakutanisha wenyeviti wa ccm ngazi ya kata pamoja na makatibu wa Ccm ngazi ya kata lengo lake kubwa ni kuweka mikakati madhubuti ya kukijenga chama chetu kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa,”
“Pamoja na kuwa katika maandalizi ya kujiandaa na kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni lazima tukawaheshimu viongozi ambao wapo madarakani na tusianze kupanga safu za viongozi wengine kabla ya muda wake hii haitakiwi kabisa,”alibainisha Mwenyekiti Nyamka.
Kadhalika aliongeza kuwa viongozi wa chama ambao wapo madarakani wanastahili kupewa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza Ilani ya chama kwa vitendo na sio kuwavunja moyo pindi wakiwa bado madarakani.
Kadhlika alisema kwamba lengo lubwa la chama ni kuweka mipango madhubuti ambayo itasaidia kushiriki kikamilifu na hatimaye kushinda kwa kishindo katika chaguzi mbali mbali ikiwemo wa serikali za mitaa ambao utafanyika mwaka huu.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo aliwakumbusha viongozi hao kuweka misingi ya kuwa na umoja na mshikamano ili kuweza kukiimarisha chama kuanzia ngazi za mashina,matawi,kata hadi ngazi za juu hali ambayo itasaidia kukijenga chama.
Katika hatua nyingine Nyamka alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka kwa kuweza kushirikiana bega kwa bega na wananchi katika kutekeleza miradi mbali mbali ya kimaendeleo.
Pia Mwalimu Nyamka hakusita kumshukuru kwa dhati Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutenga fedha ambazo zimeweza kusaidia kwa kiasi kukubwa katika kukamilisha miradi mbali mbali ya maendeleo.
Aliongeza kuwa Rais Samia ameweza kuteleza Ilani ya chama kwa vitendo ambayo imepelekea baadhi ya maeneo kuwaondolea adha changamoto ya wanakinamama kutembea umbari mrefu kwa ajili ya kufuata huduma maji safi na salama.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Kibaha mji Issack Kalleiya amewakumbusha viongozi kuwasajili wanachama kwa mfumo wa kisasa wa kidigitali ambao utasaidia katika kutambua wanachama wake.