MASHINDANO ya Mbunge Kilimo Cup yanayoshirikisha timu nane za jimbo la Singida Mashariki yameanza kutimua vumbi kwa timu ya Mawakala Fc kuwatandika vikali mahasimu wao Sokoni Fc bao mbili kwa bila.
Mashindano hayo yamefunguliwa na mbunge wa jimbo hilo Miraji Mtaturu katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Ikungi na kushirikisha viongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilaya,viongozi wa serikali na madiwani wakiongozwa na mwenyekiti wa halmashauri ya Ikungi Ally Mwanga.
Akifungua mashindano hayo Mhe Mtaturu amewataka wachezaji na wananchi kujiandaa vizuri kwenye msimu wa kilimo kwa kufuata kanuni bora za kilimo na kupanda mbegu zilizoshauriwa na wataalam ili kujitosheleza kwa chakula.
“Nawaahidi kuwa nitaendelea kufadhili mashindano kama haya ili kuwaweka vijana pamoja ikiwa ni kudumisha upendo,undugu na mshikamano,na kuunga mkono juhudi za serikali za kupambana na upatikanaji wa ajira kwa vile najua michezo ni ajira,”alisisitiza Mhe Mtaturu.
Ametoa rai kwa timu za wilaya ya Ikungi kuitikia wito wa kujisajili mapema ili kuwe na ligi ya wilaya itakayoendana na kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini(TFF) kila mwaka.
Awali akisoma taarifa ya mashindano kwa mgeni rasmi mratibu wa mashindano hayo Yassin Ntandu amesema wameamua kuandaa mashindano hayo ili kuwaweka vijana pamoja.
“Mashindano haya yanalenga kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye msimu wa kilimo chini ya kauli mbiu ya isemayo”Kilimo ni uti wa mgongo”,tunakushukuru mbunge wetu kwa kukubali kuwa mfadhili kwa kutoa zawadi kwa washindi na vifaa vya michezo kwa kila timu inayoshiriki,”alisema Ntandu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri mhe Mwanga amempongeza sana mhe mbunge kwa kuwaandalia vijana ligi ya mpira ambayo itawasaidia kuwaepusha na makundi hatarishi na kuwahamasisha kufanya kazi.
“Nimevutiwa sana na utekelezaji wa majukumu anayofanya mbunge kwani toka alipokuwa mkuu wa wilaya alifanya mambo mengi ya kimaendeleo yanayostahili kuigwa,nimuahidi kama halmashauri kuunga mkono kwenye zawadi zitakazotolewa kwa washindi.
Nae Mwenyekiti wa CCM wilaya Mika Likapakapa amempongeza sana Mhe Mtaturu kwa namna anavyoitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwenye sekta mbalimbali ikiwemo michezo kwa vitendo.
“Sisi kama chama wilaya tunaridhishwa sana na utekelezaji wa Rais wetu Mhe Dkt John Pombe Magufuli, hata kwa mbunge Mhe Mtaturu anafanya vizuri sana,niwaombe wananchi tuwape ushirikiano pamoja viongozi wa Vijiji na Vitongoji waliochaguliwa hivi karibuni ili wawaletee maendeleo zaidi,”alisema mwenyekiti huyo wa CCM wilaya.
Timu zinazoshiriki mashindano hayo ni Sokoni Fc,Mawakala Fc,Tanesco,Dung’unyi,Matare,Nkuhi,Mbwajiki na Issuna.
Zawadi zitakazotolewa ni shilingi laki 200,000 na mpira kwa mshindi wa kwanza,mshindi wa pili shilingi 150,000 na mpira,mshindi wa tatu Shilingi 100,000 na mpira,mshindi wa nne shilingi elfu 50,000 na mshindi wa tano shilingi 25,000.