Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mwanjelwa Jijini Mbeya wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuzuia, kudhibiti na kutokomeza uhalifu katika Jiji hilo.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Abdi Issango Mei 07, 2024 wakati akizungumza kwenye kikao na viongozi na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mwanjelwa.
Kamanda Issango amesema kuwa, Jeshi la Polisi linathamini mchango mkubwa unaotolewa na wafanyabiashara hivyo litaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa katika maeneo yao ya biashara ili kukuza uchumi na kipato.
Aidha, Kamanda Issango amesisitiza wafanyabiashara hao kufanya kazi kidigitali kwa kuhakikisha wanafunga kamera za usalama (CCTV) kwenye maduka yao ili kuzuia uhalifu na pindi unapotokea kurahisisha kazi ya upelelezi.
Naye, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Andrew Kantimbo amewataka wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mwanjelwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kwenda kutoa ushahidi mahakamani badala ya kudai kurejeshewa mali zao na kuomba kutoendelea na kesi hali inayopelekea watuhumiwa kuachiwa na kurudi mitaani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Anthony Mkwawa amewataka wafanyabiashara hao kushirikiana na Polisi Kata waliopo katika maeneo yao na kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ambapo vitafanya doria kwa lengo la kuzuia uhalifu.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wengine ndugu Emmanuel Ndanta amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi hasa ushirikiano toka kwa Polisi Kata na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mwanjelwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Christina Kakiziba pamoja na Askari wengine kwani umesaidia kuzuia vitendo vya uhalifu hasa uporaji na uvunjaji wa maduka.
Mbali na kutoa elimu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipata nafasi ya kusikiliza kero na changamoto toka kwa wafanyabiashara hao kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa mteja na kuimarisha ulinzi na usalama katika mazingira yao ya kazi.