Serikali imesema Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia wa Mwaka 2024 2034 kwa kiasi kikubwa utasaidia kupungua kwa vitendo vya ukataji wa miti kwa kupunguza matumizi ya nishati itokanayo na misitu.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ameliarifu Bunge wakati akijibu swali la Mbunge wa Buhigwe Mhe. Kavejuru Felix aliyeuliza kuhusu mkakati wa kukomesha ukataji holela wa miti na uchomaji moto wa misitu nchini.
Pamoja na mambo mbalimbali, Mhe. Khamis amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera, kimkakati na utekelezaji wa miradi ili kukabiliana na changamoto hizo.
Ametaja Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira 2022-2032 ambao umebainisha hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira.
Ili kuhakikisha utunzaji wa misitu unakuwa endelevu, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali inawapa elimu wananchi kutambua fursa zinazopatikana kutokana na utunzaji wa rasilimali za misitu.
Halikadhalika, Mhe. Khamis ametaja hatua zingine zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na kuendeleza na kuimarisha doria zinazofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili kulinda misitu kutokana na moto na uvunaji holela.
Kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi na jamii katika usimamizi endelevu wa misitu na Kuandaa Sheria na Miongozo ya Uvunaji na Usafirishaji wa Mazao ya Misitu katika Halmashauri zetu nchini.
Katika hatua nyingine akijibu swali la nyongeza kuhusu hatua za Serikali katika kudhbiti uchomaji wa misitu, Naibu Waziri Khamis amezielekeza Kamati za Ulinzi na Vijiji, Kata na Wilaya kuimarisha ulinzi katika misitu.