…………………
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Usalama barabarani nchini Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, ACP Michael Deleli amemtaka Mkuu wa Usalama barabarani wa mkoa wa Dodoma kutoa mafunzo ya Elimu ya usalama barabarani ya mara kwa mara kwa waendesha Bajaji na pikipiki ili wapate Elimu itakayowafanya wawe na uelewa wa kufanana katika matumizi salama na sahihi wanapotumia barabara.
ACP Deleli amesema hayo wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoa wa Dodoma ambapo aliweza kukutana na Wataalamu wa usafirishaji wanaotumia Bajaj kusafirisha abiria na ubebaji wa mizigo wa mkoa wa Dodoma.
Afande Michael Deleli alipata wasaa wa kuwapa Elimu Usalama barabarani waendesha Bajaj na Pikipiki wapatao 79, iliyohusu matumizi sahihi na salama ya barabara ili kuepusha ajali za barabarani zinazopelekea vifo na majerihi.
Aidha amewataka kutii sheria zote za Usalama barabarani bila kushurutishwa. ikiwemo kutopita taa nyekundu, kutobeba abiria zaidi ya mmoja (mishikaki), kutoendesha pikipiki na Bajaji zao kwa mwendo kasi.
‘Pia muache tabia ya ku overtake maeneo yenye kona, milima, madaraja na sehemu hatarishi, mujenge utamaduni wa kuvaa kofia ngumu/ helmeti munapoendesha pikipiki zenu barabarani’amesema ACP Deleli
Halikadhalika, Afande ametoa maelekezo kwa RTO wa mkoa wa Dodoma kuwa wakati wa utoaji wa Elimu ya usalama barabarani Kwa Kundi hili ahakikishe anashirikiana na Shule au vyuo vilivyopo mkoa wa Dodoma.
Afande Michael amewaasa madereva hawa kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mkononi mara inapojitokeza changamoto yeyote ya kusabishiwa ajali au kusababisha ajali.
Hata hivyo amewataka madereva wote kutojihusisha na vitendo vyovyote vya uhalifu na wahalifu bali wafanye kazi kwa bidii ili waweze kufikia malengo waliojiwekea.