Waziri wa Wizara ya Uchukuzi Profesa Makame Mnyaa Mbarawa akiwasilisha Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025 Bungeni leo.
Moja ya mitambo mipya ya Rada iliyofungwa na Mamlaka ya hali ya Hewa TMA kupitia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
……………………….
Katika kuhakikisha wananchi wanaishi katika hali ya utulivu pamoja na mali zao na kuchukua tahadhari mbalimbali katika majanga yanayoweza kujitokeza kutokana na hali mbaya ya hewa Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea na utoaji wa huduma, kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa hapa nchini.
Majukumu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA ni kutoa utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za hali mbaya ya hewa, kupima na kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutafiti kisayansi mabadiliko ya hali ya hewa nchini, kubadilishana taarifa za hali ya hewa katika mtandao wa mawasiliano wa dunia kulingana na makubaliano ya Kimataifa na kuiwakilisha Tanzania katika masuala ya hali ya hewa Kikanda na Kimataifa.
Akiwasilisha Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2024/2025 Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mnyaa Mbarawa amesema TMA imeendelea kutoa huduma za utabiri wa kila siku, siku kumi na ule wa muda mrefu pamoja na tahadhari ya matukio ya hali mbaya ya hewa ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao ambapo usahihi wa utabiri umefikia asilimia 86 ambao ni juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
Waziri Profesa Mbarawa ameongeza kuwa TMA ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa kuanzia tarehe 22 – 27 Januari 2024, na kuendelea kukidhi vigezo vya kumiliki cheti cha ubora (ISO 9001: 2015).
“Katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Ibara ya 59(j) na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III 2021/22-2025/26), Serikali iliahidi kuendelea kuimarisha miundombinu na huduma za hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa rada,” Amesema Profesa Mbarawa
Amelitaarifu Benge kuwa Serikali kupitia TMA imekamilisha ufungaji wa rada za hali ya hewa katika mikoa ya Kigoma na Mbeya na kufikisha jumla ya rada tano (5) za hali ya hewa nchini.
Aidha, ameongeza kuwa utengenezaji wa rada nyingine mbili (2) unaendelea kiwandani nchini Marekani na inatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2024.
Rada hizo zitafungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma na hivyo kukamilisha lengo la muda mrefu la kuwa na rada saba (7) za hali ya hewa nchini.
Amesema sambamba na hilo, Serikali imeingia mkataba wa kuboresha rada za hali ya hewa zilizofungwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza ili kuendana na teknolojia ya kisasa ya rada za hali ya hewa.
Ametanabaisha kuwa katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga, Serikali ilikamilisha ufungaji wa mitambo mitano (5) ya kutoa huduma za hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Songwe, Zanzibar, Mtwara, Arusha na Songea.
Taratibu za ufungaji wa mitambo mitatu (3) ya kupima hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Musoma, Iringa na Mpanda zinaendelea.
“Serikali imekamilisha ununuzi wa seti 28 za mitambo ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe (Automatic Weather Stations) ambapo mitambo mitatu (3) imefungwa katika vituo vya hali ya hewa vilivyopo katika viwanja vya ndege vya Mtwara, Songea na Arusha na mitambo 25 inaendelea na maandalizi ya kufungwa katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Tanga, Dodoma, Singida, Kilimanjaro, Katavi, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu, Kaskazini Unguja, Mara na Mwanza,” Amesema Profesa Mbarawa
Akizungumzia kuhusu kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kujenga uwezo kwa watumishi, Serikali kupitia TMA amesema serikali imeendelea na ujenzi wa jengo la ofisi ya Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 39.
Vilevile, watumishi 74 wanaendelea na mafunzo ndani na nje ya nchi katika ngazi mbalimbali za elimu.