NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, akizungumza na kada wa CCM ambaye pia ni mkurugenzi mstaafu idara ya umwagiliaji Wizara ya Kilimo Zanzibar Dkt.Ramadhan Aseid Ramadhan nyumbani kwake Fuoni Zanzibar.
…………………..
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa amesema Chama hicho kitaendelea kuwa mtetezi na mwangalizi wa Wananchi wote.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na kada wa CCM ambaye ni Mkurugenzi mstaafu idara ya umwagiliaji Wizara ya Kilimo Zanzibar Dkt.Ramadhan Aseid Ramadhan huko nyumbani kwake Fuoni.
Dkt.Dimwa,amesema lengo la ziara yake hiyo ni kumtembelea ili kumjulia hali ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara zake za kuwatembelea makada,wazee na wananchi kwa ujumla.
Alieleza kuwa ziara hizo zinaendeleza utamaduni wa Chama Cha Mapinduzi wa kuweka daraja huru la mahusiano mema baina ya Chama na Wananchi bila kujali tofauti za kidini,kisiasa na kikabila.
“Kila nikikutana na wazee na makada wakongwe waliotumia nguvu na muda wao kuitumikia nchi yetu kwa uadilifu nafurahi sana kwani napata ushauri,mbinu na nasaha nzuri za kunisaidia katika masuala ya utendaji na kuwatumikia kwa ufanisi zaidi wanachama wa CCM na Wananchi kwa ujumla.
Dhamira ya Chama Cha Mapinduzi ni kushinda katika uchaguzi mkuu ujao wa 2025 ili tuendelee kuongoza nchi kwa uadilifu na ufanisi mkubwa kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazoendana na mahitaji yao ya sasa kiuchumi,kijamii na kimaendeleo”,alisema Dkt.Dimwa.
Naye Mkurugenzi mstaafu idara ya umwagiliaji Wizara ya Kilimo Zanzibar Dkt.Ramadhan Aseid Ramadhan,amemshukru Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Dimwa kwa kumjali na kumtembelea kwa dhamira ya kubadilishana mawazo juu ya masuala mbalimbali ya Kijamii.
Dkt.Aseid,amempongeza kwa dhati Naibu Katibu Mkuu Dkt.Dimwa kwa utendaji wake unaoleta ufanisi na mabadiliko mkubwa ya kiutendaji ndani ya Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake.