Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Tulia Ackson,anaamua kuwapeleka kwenye darasa jjipya kabisa wanahabari, huku akiwaasa kutulia,kujitafakari na kuongeza umakini katika kazi zao.
Anasema pasipo kufanya hivyo,itakuwa vigumu kwao kukabiliana(isomeke kutoboa) na changamoto za kiteknolojia ikiwemo ujio wa akili mnemba(artificial intelligence).
Mhadhiri huyo Mwandamizi wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye sasa ni mwanasiasa, anasema katika hali ya kawaida na pasipo kuwa makini,siku hizi ni rahisi wanahabari kuingia kwenye mkumbo(isomeke kuingia mkenge)wa kusadiki habari za picha mnato,ambazo zimetengenezwa kwa mbinu na makusudi mabaya na kisha kuzisambaza kwenye vyombo vya habari na kuuaminisha umma kuwa habari hizo ni za kweli, wakati ni kinyume chake.
“Kwa mfano, katika hali hiyo,je chombo cha habari ambacho kimerusha hewani habari kama hiyo,kinawezaje kuyaondoa madhara yaliyosababishwa na upotoshaji huo?,”anahoji Spika huyo ambaye kwa sasa ni Rais wa Umoja Mabunge ya Dunia.
Anatoa changamoto hizo kwenye hotuba yake kama mgeni rasmi kwenye siku ya kwanza ya maadhmisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Mei 2 na 3 kila mwaka.
Hotuba yake hiyo anayoigeuza somo rasmi kama mhadhara wa kitaaluma,anasema kuwa ujio wa vyombo vya habari vya mtandaoni nao utawafanya Wanahabari watafakari upya maana halisi ya neno chombo cha habari.
“Hivi mtu ambaye yeye mwenyewe ndiye mmiliki wa chombo,hicho hapo hapo yeye mwenyewe ndiye mkusanyaji na mhariri wa habari hiyo,je huyu naye ni chombo cha habari?,”Anahoji na kuwaacha wanahabari wakikuna vichwa vyao.
Anaongeza kuwa ni muhimu ifike mahali jamii,kwa kusaidiwa na wanahabari wenyewe,ichore msitari kati ya maoni ya mtu binafsi na habari za zinazokusanywa na vyombo vya habari,huku kipimo sahihi kikiwa ni ubora wa habari hizo.
Anawataka Wanahabari nchini kutumia Kalamu na Kamera zao kuelimisha jamii juu ya mabadiliko ya tabia nchi sambamba na athari zake, vikiwemo vimbunga na mafuriko, ambayo tayari yametufikia hapa nchini.
Kwenye darasa lake hilo anasisitiza wanahabari kuzingatia usawa wa kijinsia wakati wa kuandika habari za uchaguzi miongoni mwa wagombea,hasa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,lakini pia akiwaacha wasikilizaji wake na maswali kadhaa.
“Je kati ya wagombea wanaochuana, je ni nani atakayepewa haki kati ya yule anayewalipia nauli wanahabari kwenda kwenye tukio na yule asiyefanya hivyo? Je uhuru wa Mwanahabari huyo aliyelipiwa usafiri ni uhuru wa kweli?Haki itatendeka kwa yule asiyetoa nauli,” anatoa changamoto hizo na kuongeza kuwa hata hivyo hakuna uhuru usiokuwa ma mipaka.
Awali, kwenye risala ya wanahabari hao iliyosomwa na Rais wa Umoja wa Vilabu vya Wanahabari nchini, Deo Nsokolo, anaiomba serikali kufuatilia madeni ambayo vyombo vya habari kwa ujumla wao vinaidai serikali, ambapo imeshindwa kuwalipa kwa muda mrefu.
Nsokolo anasema deni hilo ni jumla ya 18bn/- ambazo zinatokana na gharama za matangazo na nyinginezo zilizokopwa na serikali kwa nyakati tofauti.
Aidha, katika risala hiyo wanahabari hao wanaishukuru serikali kwa kuvifanyia marejeo vipengele 9 kati ya 12 Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, ambapo wanasema wanaomba kwamba hata vifungu hivyo vilivyobakia navyo vifanyiwe marekebisho.
Anapojibu hoja hizo, Spika wa Bunge anasema kuwa Bunge lake litawasiliana idara zote za serikali zinazodaiwa na vyombo vya habari na kuzitaka zianze kulipa madeni hayo.
“Idara zile ambazo hazitaanza kufanya hivyo mara moja zitatakiwa kuandika maelezo fulani,zikitueleza kwamba zina mpango gani na madeni hayo,”anasema.
Naye Waziri wa Habari na Mawasiliano,ambaye ndiye mwenye dhamana, Nape Nauye anasema vipengele vya sheria hivyo vilivyosalia kurekebishwa ni vile tu ambavyo serikali na wadau wa habari walikubaliana kutokukubaliana na hivyo serikali haitakuwa na nia ya kuendelea kuvibadilisha kwasasa labda hapo baadaye.
“Mheshimiwa Spika wewe unajua kwamba kuna baadhi ya vipengele hivi tulivyo vibadilisha vina nguvu yako wewe mwenyewe, maana ulikuwa unahoji kwamba kwanini tunavichelewesha. Japo tulijaribu kukueleza wasiwasi wetu,lakini ulituhimiza kuwa ni muhimu kwamba vikabadilishwa kwakuwa vinagusa maisha ya wanahabari, nasisi tulifanya hivyo,”anasema.
Waziri Nape anaamua kufafanua kuhusu hili la deni la serikali kwa vyombo vya serikali,ambapo anasema kati ya jumla hiyo 18bn/-,hizo bilioni 12 ni deni serikali kwa vyombo vya serikali,wakati kiasi kinachosalia ndilo deni la serikali kwa sekta binafsi.
Siku hii muhimu kwa wanahabari duniani inayoadhimishwa kila mwaka, hapa nchini inaandaliwa na Kamati ya Maandalizi inayohusisha taasisi mbalimbali za waandishi wa habari pamoja na wadau wao,huku taasisi mojawapo kati ya hizo ikipewa jukumu la kuongoza maandalizi hayo.
Mwaka huu taasisii iliyopewa jukumu la kusimamia maandalizi hayo ni Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari nchini (UTPC) na ikihudhuriwa ma Wanahabari zaidi ya 300 kutoka nchi nzima.UTPC yenyewe inao wawakilishi kutoka vilabu 28 nchini,kati ya hizo,2 zinatoka Tanzania Visiwani.
Taasisi zingine zilizoshiriki maandalizi hayo ni Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali,Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania(UN in Tanzania),Shirika la Elimu na Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa(UNESCO),Mfuko wa Kimataifa wa Watoto(UNICEF)Baraza la Habari(MCT).
Zingine ni OJADACT,Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), IMS, BBC MEDIA ACTION,JET, ELIMIKA WEEKEND, Mfuko wa Habari Tanzania (TMF),Shirika la Waandishi wa Habari Kusini mwa Afrika(MISA Tanzania), Jukwaa la Wahariri(TEF), NUKTA AFRICA, JAMII FORUMS, TWAWEZA, TADIO, Kituo cha Haki za Binadamu chini(LHRC),JOWUTA, LSF.
Wadau wengine ambao siyo taasisi za kihabari waliofadhili kusanyiko hilo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Mamlaka ya Udhiti huduma za Umeme na Maji(EWURA)Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Umma(PSSSF), na wa Shirika la Umeme nchini(Tanesco),Benki ya NMB,Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) na Kampuni mbili za tumbaku yaani Alliance one na Mkwawa Leaf na Kampuni mama ya ASAS pamoja kampuni zake tanzu(ASAS GROUP).
Mwisho wa mhadhara huu wa Dk Tulia, wanahabari wanamshukuru Mgeni huyu kwa ujio wake kwa kumpa tuzo muhimu inayokabidhiwa kwake na Rais wa UTPC, Deo Nsokolo, akiambatana na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi.