Kaimu Mkurugenzi na Muendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Dkt. Kanael Nnko akizungumza jambo katika hafla ya kufunga mafunzo ya Wataalam kutoka Benki washirika kuhusu namna bora kutoa mikopo katika sekta ya kilimo iliyofanyika leo Mei 3, 2024 katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Ephraim Mwasanguti akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kutoa mafunzo kwa wataalam kutoka Benki washirika kuhusu namna bora ya kutoa mikopo katika sekta ya kilimo.
Meneja Mahusiano Kitengo cha wateja wakubwa Benki ya ABSA Mollen Charles akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa mafunzo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Meneja Uhusiano Kilimo Biashara Benki ya CRDB Salvatory Sylvester akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa mafunzo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kaimu Mkurugenzi na Muendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Dkt. Kanael Nnko (wa pili kutoka kulia) akiwakabidhi vyeti wahitimu wa mafunzo hayo kutoka benki mbalimbali zilizoshiriki.
…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imefunga mafunzo kwa wataalam 52 kutoka Benki washirika kuhusu namna bora kutoa mikopo katika sekta ya kilimo pamoja na kuangalia viatarishi jambo ambalo litasaidia taasisi za fedha kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta tija kwa Taifa.
Mafunzo hayo yameendeshwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia BoT Academy kwa lengo la kuzalisha wataalam wengi katika taasisi za fedha ambao watasaidia kutoa mikopo.
Akizungumza leo Mei 3, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya wataalam ya kutoa mikopo katika sekta ya kilimo, Kaimu Mkurugenzi na Muendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Dkt. Kanael Nnko, amesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuleta tija katika utoaji wa mikopo sekta ya kilimo.
Dkt. Nnko amesema kuwa lengo ni kuhakikisha idadi kubwa ya wakulima wanafikiwa na kupata mikopo katika Mikoa yote kwa maendeleo ya Taifa.
“Tunaamini mafunzo haya pamoja na washiriki yanakwenda kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yetu ya hakikisha sekta ya kilimo inasonga mbele” amesema Dkt. Nnko.
Amesema kuwa TADB katika kipindi cha miaka sita mpaka sasa mfuko wa dhamana ya Benki ya Kilimo imeweza kudhamini mikopo ya shilingi bilioni 270 kupitia benki washirika.
Ameeleza kuwa wameweza kuwafikia wakulima walengwa 24,000, huku benki ya washirika wametoa asilimia 11 ya mkopo katika sekta ya kilimo na kuendelea kuongeza juhudi ili kufikia mwaka 2030 sekta ya mikopo ili imefika asilimia 30.
“Kilimo ni sekta kubwa hivyo huwezi kuwafikia wote kwa siku moja, juhudi zinaendelea kufanyika ili vijana, wakina mama na baba waweze kuingia katika sekta ya kilimo” amesema.
Amefafanua kuwa mafunzo hayo yameendeshwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia BoT Academy pamoja na washirika wengine kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) pamoja na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) ambao wameshiriki katika kuunda mifumo pamoja na kufundisha.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Ephraim Mwasanguti, amesema kuwa miongoni mwa majukumu yao ni kutoa elimu kwa mabenki na taasisi za fedha kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali.
Dkt. Mwasanguti amesema kuwa lengo la mafunzo ni kutoa elimu kwa maafisa wa mikopo ili waweze kutoa mikopo ambayo italipika na kuleta matokeo chanya katika sekta ya kilimo.
“Tulipewa kazi na benki ya maendeleo ya kilimo ya kutengeneza programu kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo hasa ikilenga kuelimisha mabenki hasa maafisa mikopo ili waweze kutoa mikopo ambayo italipika kwa sababu hizi ni fedha za umma na kuleta matokeo mazuri katika nchi yetu” amesema Dkt. Mwasanguti.
Nao baadhi ya wahitimu wakiwemo Meneja Mahusiano Kitengo cha wateja wakubwa ABSA Benki Mollen Charles pamoja na Meneja Uhusiano Kilimo Biashara Benki ya CRDB Salvatory Sylvester, wamesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuwasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.