Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
Mei 3
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Mzava, amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuongeza kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa kiwanda cha makaa ya mawe, kata ya Visegese wilayani Kisarawe, Mkoani Pwani kabla ya Mei 30 , mwaka huu.
Mradi huo ambao ukikamilika utagharimu sh.bilioni 2.4 kati ya fedha hiyo bilioni 1.2 ni kwa ajili ya kununua mtambo na bilioni 1.2 ujenzi na vifaa, unatakiwa kukamilika kabla ya Mei 30, 2024 ,ambapo umefikia asilimia 60 bado asilimia 40 na utazalisha tani 20 kwa saa za mkaa mbadala.
Akikagua kiwanda hicho cha makaa ya mawe , Mzava alieleza lengo la mradi huo ni kutengeneza nishati mbadala ambayo itakuwa mkombozi wa mazingira na watumiaji wa nishati kwasababu ni nishati rafiki kiafya na kimazingira.
“Agenda yetu ya msingi kabisa katika Mwenge wa Uhuru 2024 kuhusu Uhifadhi wa mazingira na uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Uhifadhi wa mazingira, tunavyokwenda na mabadiliko ya kutoka kwenye nishati isiyo rafiki” alifafanua Mzava.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt Seleman Jafo alieleza mradi huo ni muhimu katika kutunza mazingira.
“Tukumbuke nchi yetu inapoteza miti zaidi ya hekta 400,000 ,hii ni changamoto kubwa Kitaifa.”
“Ndio maana Rais Dkt Samia katika mkutano wake alipokuwa na akinamama alihimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia,halikadhalika Makamu wa Rais Philip Mpango wakati wa maadhimisho ya STAMICO aliwaelekeza waanze mpango wa kutengeneza nishati mbadala”
“Na bahati nzuri kuna timu yetu ya NEMC inafuatilia maeneo haya yote, lengo kubwa ni kuona Tanzania tunaenda kuhakikisha utunzaji wa mazingira ni jambo la msingi”
Akipokea Mwenge wa Uhuru Mei 3 mwaka huu, eneo la Kiluvya Madukani, ukitokea Kibaha,Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Fatma Nyangasa, alieleza mradi huo ni mkubwa na utachagiza matumizi ya nishati salama na kuondokana na kukata kuni,miti ovyo.
Akielezea miradi iliyopitiwa na Mwenge anasema , miradi ni 7 yenye thamani ya sh. bilioni 3.4.
Kati ya miradi hiyo , mradi mwingine ni kupanda miti na kukagua zoezi la upandaji miti shule ya Sekondari Kisarawe na kuzindua jengo la mama na mtoto kata ya Masaki.